2 Fal 5:15-27
2 Fal 5:15-27 SUV
Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako. Lakini akasema, Kama BWANA aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa. Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa BWANA. Jambo hili BWANA amwachilie mtumwa wako; bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni ili aabudu humo, naye akitegemea mkononi mwangu, nami nikijiinama nyumbani mwa Rimoni, hapo ninapojiinama nyumbani mwa Rimoni, BWANA amwachilie mtumwa wako jambo hili. Akamwambia, Enenda kwa amani Basi akamwondokea mbali kidogo. Lakini Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama BWANA aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake. Basi Gehazi akamfuata Naamani. Naye Naamani, alipoona mtu apigaye mbio anakuja nyuma yake, alishuka garini amlaki, akasema, Je! Ni amani? Akasema, Amani. Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana na manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili. Naamani akasema, Uwe radhi, ukatwae talanta mbili. Akamshurutisha, akafunga talanta mbili za fedha ndani ya mifuko miwili, na mavazi mawili, akawatwika watumishi wake wawili; nao wakayachukua mbele yake. Naye alipofika kilimani, alivitwaa mikononi mwao, akaviweka nyumbani; akawaacha wale watu kuondoka, nao wakaenda zao. Lakini yeye akaingia, akasimama mbele ya bwana wake. Elisha akamwambia, Watoka wapi, Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali. Akamwambia, Je! Moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng’ombe, na watumwa, na wajakazi? Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele. Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji.