2 Wafalme 5:15-27
2 Wafalme 5:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndipo akarudi kwa mtu wa Mungu pamoja na watu wake, akasema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu yeyote ila tu Mungu wa Israeli; kwa hiyo, tafadhali sasa upokee zawadi za mtumishi wako.” Elisha akajibu, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai ambaye ninamtumikia, kwamba sitapokea zawadi yoyote.” Naamani akamsihi, lakini Elisha akakataa kabisa. Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea zawadi zangu, basi tafadhali umpatie mtumishi wako udongo unaoweza kubebwa na nyumbu wawili, kwani toka leo mimi mtumishi wako sitatoa sadaka za kuteketezwa wala tambiko kwa miungu mingine ila tu kwa Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu na anisamehe ninapofuatana na mfalme wangu kwenda kuabudu katika hekalu la Rimoni mungu wa Aramu. Naomba Mwenyezi-Mungu anisamehe!” Elisha akamwambia, “Nenda kwa amani.” Naamani akaenda zake. Alipokuwa bado hajaenda mbali, Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, “Tazama, bwana wangu amemwachilia Naamani Mwaramu aende bila kupokea chochote alicholeta. Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo nitamfuata ili nipate kitu kutoka kwake.” Hapo akaondoka kumfuata Naamani. Naamani alipotazama na kuona mtu anamfuata mbio, akashuka garini mwake akaenda kukutana naye. Basi, akamwuliza, “Je, kuna usalama?” Gehazi akajibu, “Mambo yote ni sawa ila tu bwana wangu amenituma nikuambie kwamba sasa hivi amepokea watu wawili wa kundi la manabii katika nchi ya milima ya Efraimu, naye angependa uwape vipande 3,000 vya fedha na mavazi mawili ya sikukuu.” Naamani akasema, “Tafadhali chukua vipande 6,000 vya fedha.” Akamsihi, kisha akamfungia mafungu mawili na kumpa mavazi mawili ya sikukuu, akawapa watumishi wake wawili na kuwaagiza wafuatane na Gehazi. Walipofika mlimani alipoishi Elisha, Gehazi akachukua mafungu ya fedha kutoka kwa watumishi wa Naamani na kuyapeleka ndani, nyumbani mwake. Kisha akawaruhusu wale watumishi waende zao, nao wakaondoka. Halafu Gehazi akaingia nyumbani kwa Elisha na kuanza kumhudumia. Elisha akamwuliza, “Ulikwenda wapi?” Gehazi akajibu, “Sikuenda mahali popote.” Lakini Elisha akamwambia, “Kwani roho yangu haikuwa pamoja nawe wakati mtu yule alipotoka garini mwake na kuja kukutana nawe? Je, huu ndio wakati wa kupokea fedha na mavazi, mashamba ya mizeituni na mizabibu, kondoo na ng'ombe au watumishi wa kiume na wa kike? Kwa hiyo ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazawa wako milele.” Basi, Gehazi aliondoka akiwa tayari ameshikwa na ukoma, na ngozi yake ilikuwa nyeupe kama theluji.
2 Wafalme 5:15-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani kote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee zawadi kutoka mtumwa wako. Lakini akasema, Kama BWANA aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa. Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa BWANA. Jambo hili BWANA amwachilie mtumwa wako; bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni ili aabudu humo, naye akitegemea mkononi mwangu, nami nikijiinama nyumbani mwa Rimoni, hapo ninapojiinama nyumbani mwa Rimoni, BWANA amwachilie mtumwa wako jambo hili. Elisha akamwambia, Nenda kwa amani. Lakini Naamani alipokuwa ameenda mbali kidogo, Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama BWANA aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake. Basi Gehazi akamfuata Naamani. Naye Naamani, alipoona mtu apigaye mbio anakuja nyuma yake, alishuka garini amlaki, akasema, Je! Ni amani? Akasema, Amani. Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana na manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili. Naamani akasema, Uwe radhi, ukatwae talanta mbili. Akamsihi, akafunga talanta mbili za fedha ndani ya mifuko miwili, na mavazi mawili, akawatwika watumishi wake wawili; nao wakatangulia mbele yake wakiwa wameyabeba. Naye alipofika kilimani, alivichukua kutoka mikononi mwao, akaviweka nyumbani; akawaacha wale watu kuondoka, nao wakaenda zao. Lakini yeye akaingia, akasimama mbele ya bwana wake. Elisha akamwambia, Watoka wapi, Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali. Akamwambia, Je! Moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi? Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele. Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji.
2 Wafalme 5:15-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako. Lakini akasema, Kama BWANA aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa. Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa BWANA. Jambo hili BWANA amwachilie mtumwa wako; bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni ili aabudu humo, naye akitegemea mkononi mwangu, nami nikijiinama nyumbani mwa Rimoni, hapo ninapojiinama nyumbani mwa Rimoni, BWANA amwachilie mtumwa wako jambo hili. Akamwambia, Enenda kwa amani Basi akamwondokea mbali kidogo. Lakini Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama BWANA aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake. Basi Gehazi akamfuata Naamani. Naye Naamani, alipoona mtu apigaye mbio anakuja nyuma yake, alishuka garini amlaki, akasema, Je! Ni amani? Akasema, Amani. Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana na manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili. Naamani akasema, Uwe radhi, ukatwae talanta mbili. Akamshurutisha, akafunga talanta mbili za fedha ndani ya mifuko miwili, na mavazi mawili, akawatwika watumishi wake wawili; nao wakayachukua mbele yake. Naye alipofika kilimani, alivitwaa mikononi mwao, akaviweka nyumbani; akawaacha wale watu kuondoka, nao wakaenda zao. Lakini yeye akaingia, akasimama mbele ya bwana wake. Elisha akamwambia, Watoka wapi, Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali. Akamwambia, Je! Moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng’ombe, na watumwa, na wajakazi? Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele. Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji.
2 Wafalme 5:15-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Naamani na wahudumu wake wote wakarudi kwa yule mtu wa Mungu. Akasimama mbele yake na kusema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu katika ulimwengu wote isipokuwa katika Israeli. Tafadhali sasa upokee zawadi kutoka kwa mtumishi wako.” Nabii akajibu, “Hakika kama BWANA aishivyo, ambaye ninamtumikia, sitapokea kitu hata kimoja.” Ingawa Naamani alimsihi sana, yeye alikataa. Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea, tafadhali mtumishi wako na apewe udongo kiasi cha mzigo wa kuweza kubebwa na punda wawili, kwa sababu mtumishi wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa na dhabihu kwa mungu mwingine isipokuwa BWANA. Lakini BWANA na amsamehe mtumishi wake kwa kitu hiki kimoja: Wakati bwana wangu atakapoingia kwenye hekalu la Rimoni ili kusujudu, naye akiwa anauegemea mkono wangu, nami nikasujudu huko pia, wakati nitakaposujudu ndani ya hekalu la Rimoni, BWANA na amsamehe mtumishi wako kwa ajili ya jambo hili.” Elisha akamwambia, “Nenda kwa amani.” Baada ya Naamani kusafiri umbali fulani, Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akajiambia mwenyewe, “Bwana wangu amemwachia kirahisi sana Naamani, huyu Mwaramu, kwa kutokupokea kutoka kwake vile alivyovileta. Hakika kama BWANA aishivyo, nitamkimbilia na kupata kitu kutoka kwake.” Hivyo Gehazi akaharakisha kumfuatilia Naamani. Naamani alipomwona akikimbia kumwelekea, akashuka chini kutoka kwenye gari lake na kwenda kumlaki. Akauliza, “Je, mambo yote ni sawa?” Gehazi akajibu, “Mambo yote ni sawa. Bwana wangu amenituma nikuambie, ‘Vijana wawili kutoka kwa wana wa manabii wamenijia kutoka nchi ya vilima ya Efraimu. Tafadhali wape talanta ya fedha na mivao miwili ya mavazi.’ ” Naamani akasema, “Hakika, chukua talanta mbili za fedha.” Akamsihi Gehazi azipokee, kisha akafunga talanta mbili za fedha katika mifuko miwili pamoja na mivao miwili ya mavazi. Akawapa watumishi wake wawili mizigo hiyo, nao wakaibeba wakitangulia mbele ya Gehazi. Gehazi alipofika kwenye kilima, akavichukua vile vitu kutoka kwa wale watumishi na kuvificha ndani ya nyumba. Akawaaga wale watu, nao wakaondoka. Kisha akaingia ndani na kusimama mbele ya Elisha bwana wake. Elisha akamuuliza, “Gehazi, ulikuwa wapi?” Gehazi akajibu, “Mtumishi wako hakwenda popote.” Lakini Elisha akamwambia, “Je, roho yangu haikuwa pamoja nawe wakati yule mtu aliposhuka kutoka kwenye gari lake ili kukulaki? Je, huu ni wakati wa kupokea fedha au kupokea nguo, mashamba ya mizeituni, mashamba ya mizabibu, makundi ya kondoo na mbuzi, makundi ya ngʼombe, au watumishi wa kiume na wa kike? Ukoma wa Naamani utakushika wewe na wazao wako milele.” Kisha Gehazi akaondoka mbele ya Elisha, mwenye ukoma, mweupe kama theluji.