2 Fal 17:24-41
2 Fal 17:24-41 SUV
Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake. Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha BWANA; kwa hiyo BWANA akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao. Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi. Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi. Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha BWANA. Lakini pamoja na hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao walimokaa. Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima, Waavi wakafanya Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. Basi hivyo wakamcha BWANA, nao wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia dhabihu katika nyumba za mahali pa juu. Wakamcha BWANA, na kuitumikia miungu yao wenyewe, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao. Hata siku hii ya leo hufanya sawasawa na kawaida za kwanza; wala hawamwogopi BWANA, wala hawazifuati sheria zao, wala hukumu zao, wala ile torati, wala ile amri BWANA aliyowaamuru wana wa Yakobo, ambaye alimpa jina la Israeli; hao ambao BWANA alifanya agano nao, akawaamuru, akasema, Msiche miungu mingine, wala kuisujudia, wala kuitumikia, wala kuitolea sadaka; ila yeye BWANA, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri kwa nguvu nyingi, na kwa mkono ulionyoshwa, yeye ndiye mtakayemcha, yeye ndiye mtakayemsujudia, yeye ndiye mtakayemtolea sadaka; na sheria, na hukumu, na torati, na amri, alizowaandikia, hizo ndizo mtakazozishika na kuzifanya hata milele; wala msiche miungu mingine. Na hilo agano nililofanya nanyi, msilisahau; wala msiche miungu mingine; lakini BWANA, Mungu wenu, ndiye mtakayemcha; naye atawaokoa mikononi mwa adui zenu wote. Walakini hawakusikia, bali wakafanya sawasawa na kawaida zao za kwanza. Basi mataifa hawa wakamcha BWANA, tena wakaziabudu sanamu zao za kuchongwa; na wana wao vile vile, na wana wa wana wao; kama walivyofanya baba zao, wao nao hufanya vivyo hivyo hata leo.