Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 17:24-41

2 Wafalme 17:24-41 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha mfalme wa Ashuru akachukua watu kutoka Babuloni, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria mahali pa watu wa Israeli waliopelekwa uhamishoni. Wakaitwaa miji hiyo na kukaa humo. Basi ilitokea kwamba walipoanza kukaa humo, hawakumwabudu Mwenyezi-Mungu, kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akatuma simba miongoni mwao, nao wakawaua baadhi yao. Halafu watu walimwambia mfalme wa Ashuru, “Mataifa uliyochukua na kuyaweka katika miji ya Samaria hayakujua hukumu za Mungu wa nchi hiyo, kwa hiyo Mungu huyo alituma simba ambao wanawaua.” Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru, “Mrudishe kuhani mmoja kati ya wale tuliowaleta mateka; mrudishe aende na kukaa huko, ili awafundishe watu sheria ya Mungu wa nchi hiyo.” Kwa hiyo mmoja wa makuhani waliotekwa nyara toka Samaria alikwenda na kukaa Betheli, na huko aliwafundisha watu jinsi ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Lakini mataifa yote katika miji yalimoishi yalijitengenezea miungu yao na kuiweka mahali pa juu ambako watu wa Samaria walikuwa wametengeneza. Watu wa Babuloni walitengeneza vinyago vya Sukoth-benothi; Wakuthi vinyago vya Nergali; Wahamathi vinyago vya Ashima; Waiva vinyago vya Nibhazi na Tartaki; na Wasefarvaimu walitoa watoto wao kuwa sadaka za kuteketezwa kwa miungu yao Adrameleki na Anameleki. Watu hawa vilevile walimwabudu Mwenyezi-Mungu. Waliteua kutoka kati yao watu wa kila aina na kuwafanya makuhani kutumika katika mahali pa juu na kutoa sadaka huko kwa niaba yao. Hivi walimwabudu Mwenyezi-Mungu, lakini wakati huohuo waliwaabudu pia miungu yao waliyoichukua kutoka nchi zao. Hata sasa wanatenda kama walivyofanya hapo awali. Hawamwabudu Mwenyezi-Mungu, na wala hawafuati masharti, maagizo, sheria au amri ambazo yeye Mwenyezi-Mungu aliwaamuru wana wa Yakobo; ambaye alimpa jina Israeli. Mwenyezi-Mungu alikuwa amefanya agano nao na kuwaamuru, “Msiabudu miungu mingine; msiisujudie, msiitumikie wala msiitambikie. Mtaniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, ambaye niliwatoa huko Misri kwa uwezo na nguvu nyingi. Mtanisujudia mimi na kunitolea sadaka. Wakati wote mtatii masharti, maongozi, sheria na amri ambazo niliandika kwa ajili yenu, siku zote mtakuwa waangalifu kuzitenda. Msiiabudu miungu mingine, wala msisahau agano nililofanya nanyi; msiiabudu miungu mingine, bali mtaniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nami nitawaokoa kutoka mikononi mwa adui zenu.” Lakini watu hao hawakusikiliza, bali waliendelea kutenda kama walivyofanya hapo awali. Basi mataifa haya yalimwabudu Mwenyezi-Mungu, lakini pia yalitumikia sanamu zao za kusubu; na mpaka sasa hivi, wazawa wao wanaendelea kutenda hivyo kama walivyotenda babu zao.

2 Wafalme 17:24-41 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake. Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha BWANA; kwa hiyo BWANA akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao. Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi. Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi. Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha BWANA. Lakini pamoja na hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao walimokaa. Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima, Waavi wakafanya Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. Basi hivyo wakamcha BWANA, nao wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia dhabihu katika nyumba za mahali pa juu. Wakamcha BWANA, na kuitumikia miungu yao wenyewe, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao. Hata siku hii ya leo hufanya sawasawa na kawaida za kwanza; wala hawamwogopi BWANA, wala hawazifuati sheria zao, wala hukumu zao, wala ile torati, wala ile amri BWANA aliyowaamuru wana wa Yakobo, ambaye alimpa jina la Israeli; hao ambao BWANA alifanya agano nao, akawaamuru, akasema, Msiche miungu mingine, wala kuisujudia, wala kuitumikia, wala kuitolea sadaka; ila yeye BWANA, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri kwa nguvu nyingi, na kwa mkono ulionyoshwa, yeye ndiye mtakayemcha, yeye ndiye mtakayemsujudia, yeye ndiye mtakayemtolea sadaka; na sheria, na hukumu, na torati, na amri, alizowaandikia, hizo ndizo mtakazozishika na kuzifanya hata milele; wala msiche miungu mingine. Na hilo agano nililofanya nanyi, msilisahau; wala msiche miungu mingine; lakini BWANA, Mungu wenu, ndiye mtakayemcha; naye atawaokoa mikononi mwa adui zenu wote. Walakini hawakusikia, bali wakafanya sawasawa na kawaida zao za kwanza. Basi mataifa hawa wakamcha BWANA, tena wakaziabudu sanamu zao za kuchongwa; na wana wao vile vile, na wana wa wana wao; kama walivyofanya baba zao, wao nao hufanya vivyo hivyo hata leo.

2 Wafalme 17:24-41 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

2 Wafalme 17:24-41 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mfalme wa Ashuru akawaleta watu kutoka Babeli, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria badala ya Waisraeli. Wakaimiliki Samaria na kuishi katika miji yake. Wakati walianza kuishi humo, hawakumwabudu BWANA, kwa hiyo akatuma simba miongoni mwao, wakawaua baadhi ya watu. Habari ikapelekwa kwa mfalme wa Ashuru, kusema: “Watu uliowahamisha na kuwaweka katika miji ya Samaria hawajui kile Mungu wa nchi hiyo anachokitaka. Ametuma simba miongoni mwao, ambao wanawaua, kwa sababu watu hawajui anachokitaka.” Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru hivi: “Mtwae mmoja wa makuhani uliowachukua mateka kutoka Samaria ili arudi kuishi humo na awafundishe watu kile ambacho Mungu wa nchi anataka.” Basi mmoja wa makuhani ambaye alikuwa amepelekwa uhamishoni kutoka Samaria akaja kuishi Betheli na kuwafundisha jinsi ya kumwabudu BWANA. Hata hivyo, kila kikundi cha taifa lililoletwa Samaria kilitengeneza miungu yao wenyewe katika miji kadhaa mahali walipoishi, nao wakaiweka mahali pa ibada za miungu ambapo watu wa Samaria walikuwa wametengeneza katika mahali pa juu. Watu kutoka Babeli wakamtengeneza Sukoth-Benothi kuwa mungu wao, watu kutoka Kutha wakamtengeneza Nergali, na watu kutoka Hamathi wakamtengeneza Ashima; Waavi wakatengeneza Nibhazi na Tartaki, nao Wasefarvi wakachoma watoto wao kama kafara kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. Walimwabudu BWANA, lakini pia waliteua aina zote za watu wao ili kuwawakilisha kama makuhani katika mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu pa ibada. Walimwabudu BWANA, lakini pia waliitumikia miungu yao kulingana na desturi za mataifa walikotoka. Mpaka leo wanashikilia desturi zao za zamani. Hawamwabudu BWANA wala kuzishika hukumu na maagizo, sheria na amri ambazo BWANA aliwapa uzao wa Yakobo, ambaye alimwita Israeli. Wakati BWANA alipofanya Agano na Waisraeli, aliwaamuru akisema: “Msiiabudu miungu mingine yoyote wala kuisujudia, wala kuitumikia wala kuitolea dhabihu. Bali imewapasa kumwabudu BWANA aliyewapandisha kutoka Misri kwa uwezo wake mkuu na kwa mkono wake ulionyooshwa. Kwake yeye mtasujudu na kwake yeye mtatoa dhabihu. Imewapasa daima kuwa waangalifu kutunza hukumu na maagizo, sheria na amri alizowaandikia. Msiabudu miungu mingine. Msisahau agano nililofanya nanyi, wala msiabudu miungu mingine. Bali, mtamwabudu BWANA Mungu wenu, kwani yeye ndiye atakayewakomboa kutoka mikononi mwa adui zenu wote.” Hata hivyo hawakusikiliza, lakini waliendelea na desturi zao za awali. Hata wakati watu hawa walipokuwa wanamwabudu BWANA, walikuwa bado wakitumikia sanamu zao. Mpaka leo watoto wao na watoto wa watoto wao wanaendelea kufanya kama baba zao walivyofanya.