2 Fal 15:1-16
2 Fal 15:1-16 SUV
Katika mwaka wa ishirini na saba wa Yeroboamu mfalme wa Israeli Uzia mwana wa Amazia mfalme wa Yuda akaanza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, kama yote aliyoyafanya babaye Amazia. Ila mahali pa juu hapakuondolewa, nao watu wakaendelea kutoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. BWANA akampiga mfalme, akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya pekee. Na Yothamu mwana wa mfalme alikuwa juu ya nyumba, akiwahukumu watu wa nchi. Basi mambo yote ya Uzia yaliyosalia, nayo yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Uzia akalala na babaze; wakamzika pamoja na babaze mjini mwa Daudi; na Yothamu mwanawe akatawala mahali pake. Katika mwaka wa thelathini na nane wa Uzia mfalme wa Yuda Zekaria mwana wa Yeroboamu akatawala juu ya Israeli katika Samaria miezi sita. Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA kama walivyofanya babaze; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli. Na Shalumu mwana wa Yabeshi akafanya fitina juu yake, akampiga mbele ya watu, akamwua, akatawala mahali pake. Basi mambo yote ya Zekaria yaliyosalia, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli. Hilo ndilo neno la BWANA alilomwambia Yehu, akisema, Wana wako watakaa kitini mwa Israeli hata kizazi cha nne. Ikawa vivyo hivyo. Huyo Shalumu mwana wa Yabeshi alianza kutawala katika mwaka wa thelathini na kenda wa Uzia mfalme wa Yuda; akatawala muda wa mwezi mmoja katika Samaria. Menahemu mwana wa Gadi akapanda kutoka Tirza, akaja Samaria, akampiga Shalumu mwana wa Yabeshi huko Samaria, akamwua, akatawala mahali pake. Basi mambo yote ya Shalumu yaliyosalia, na fitina aliyoifanya, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli. Ndipo Menahemu akapiga Tifsa, na wote waliokuwamo, na mipaka yake, toka Tirza; kwa sababu hawakumfungulia, kwa hiyo akaupiga; nao wanawake wote waliokuwamo wenye mimba akawapasua.