2 Wafalme 15:1-16
2 Wafalme 15:1-16 NEN
Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Azaria mwana wa Amazia mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na miwili. Mama yake aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. Akatenda yaliyo mema machoni pa BWANA, kama Amazia baba yake alivyofanya. Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. BWANA akampiga mfalme kwa ukoma mpaka siku aliyokufa, naye aliishi katika nyumba iliyotengwa peke yake. Yothamu mwana wa mfalme akawa msimamizi wa jumba la mfalme, na akawatawala watu wa nchi. Matukio mengine ya utawala wa Azaria na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Azaria akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa karibu nao katika Mji wa Daudi, na Yothamu mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Zekaria mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, naye akatawala miezi sita. Akafanya maovu machoni pa BWANA, kama baba zake walivyofanya. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda. Shalumu mwana wa Yabeshi akafanya shauri baya dhidi ya Zekaria. Akamshambulia mbele ya watu, akamuua na kuingia mahali pake kuwa mfalme. Matukio mengine ya utawala wa Zekaria yameandikwa kwenye kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. Kwa hiyo neno la BWANA lililonenwa kwa Yehu likatimia, kwamba, “Wazao wako wataketi juu ya kiti cha enzi cha Israeli hadi kizazi cha nne.” Shalumu mwana wa Yabeshi akawa mfalme katika mwaka wa thelathini na tisa wa Uzia mfalme wa Yuda, naye akatawala katika Samaria kwa mwezi mmoja. Kisha Menahemu mwana wa Gadi akaenda kutoka Tirsa mpaka Samaria. Akamshambulia Shalumu mwana wa Yabeshi huko Samaria, akamuua na kuingia mahali pake kuwa mfalme. Matukio mengine ya utawala wa Shalumu, na mauaji aliyoyafanya, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. Wakati ule, akianzia Tirsa, Menahemu alishambulia Tifsa na kila mtu ndani yake, na wale waliokuwa maeneo jirani, kwa sababu walikataa kufungua malango yao. Akaiangamiza Tifsa yote, na kuwapasua matumbo wanawake wote wenye mimba.