Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Sam 18:1-16

1 Sam 18:1-16 SUV

Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe. Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake. Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia. Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli. Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu. Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye BWANA alikuwa pamoja naye. Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa. Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao.

Soma 1 Sam 18

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Sam 18:1-16

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha