Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 18:1-16

1 Samweli 18:1-16 NEN

Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe. Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake. Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe. Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake. Lolote Sauli alilomtuma Daudi kufanya, alitenda kwa hekima, hata Sauli akampa cheo cha juu katika jeshi. Jambo hili likawapendeza watu wote, hata maafisa wa Sauli pia. Watu walipokuwa wanarudi nyumbani baada ya Daudi kumuua yule Mfilisti, wanawake wakaja kutoka pande zote za miji ya Israeli kumlaki Mfalme Sauli kwa kuimba na kucheza, kwa nyimbo za furaha na kwa matari na zeze. Walipokuwa wanacheza, wakaimba: “Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake.” Sauli akakasirika sana; sehemu hii ya kurudia rudia ya wimbo huu ilimkasirisha sana. Akafikiri kuwa, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa elfu tu. Apate nini zaidi isipokuwa ufalme?” Kuanzia wakati ule na kuendelea Sauli akawa na jicho la wivu juu ya Daudi. Kesho yake roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikaja kwa nguvu juu ya Sauli. Alikuwa akitabiri nyumbani mwake, wakati Daudi alikuwa akipiga kinubi, kama alivyozoea. Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake; akautupa kwa nguvu, akijiambia mwenyewe, “Nitamchoma kwa mkuki abaki hapo ukutani.” Lakini Daudi akamkwepa mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja na Daudi, lakini alikuwa amemwacha yeye. Kwa hiyo Sauli akamwondoa Daudi mbele yake na kumpa kuwa kiongozi wa watu elfu moja, naye Daudi akatoka na kuingia akiongoza vikosi katika vita. Katika kila kitu alichofanya, Daudi alipata mafanikio makubwa, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye. Sauli alipoona jinsi alivyokuwa akifanikiwa, akamwogopa. Lakini Israeli wote na Yuda walimpenda Daudi, kwa sababu ndiye alikuwa akiwaongoza katika vita vyao.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Samweli 18:1-16