1 Fal 18:22-46
1 Fal 18:22-46 SUV
Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa BWANA; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng’ombe wawili; wao na wajichagulie ng’ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng’ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la BWANA; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri. Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng’ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini. Wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya. Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe. Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika. Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia. Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la BWANA na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni. Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu. Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji. Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu, BWANA ndiye Mungu. Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko. Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele. Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba. Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie. Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli. Mkono wa BWANA ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuiingia Yezreeli.