1 Wafalme 18:22-46
1 Wafalme 18:22-46 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo, Elia akawaambia, “Mimi tu ndiye peke yangu nabii wa Mwenyezi-Mungu niliyebaki, lakini manabii wa Baali wapo 450. Haya! Leteni fahali wawili; manabii wa Baali wajichagulie fahali mmoja, wamchinje, wamkate vipandevipande na kumweka juu ya kuni, bila kuwasha moto. Nami pia nitamtwaa huyo fahali mwingine, nitamchinja na kumweka juu ya kuni bila kuwasha moto. Kisha, wao watamwomba mungu wao, nami nitamwomba Mwenyezi-Mungu. Mungu atakayejibu kwa kuleta moto, huyo ndiye Mungu wa kweli.” Na hapo umati wote ukasema, “Naam! Na iwe hivyo.” Kisha, Elia akawaambia manabii wa Baali, “Nyinyi ni wengi; basi anzeni. Jichagulieni fahali, mtayarisheni na kumwomba mungu wenu, lakini msiwashe moto.” Hao manabii wakamtwaa fahali wao waliyepewa, wakamtayarisha, kisha wakaanza kumlilia Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakirukaruka na kuyumbayumba kuizunguka madhabahu waliyotengeneza wakisema: “Ee Baali, utusikie!” Lakini hapakutokea sauti yoyote, wala hakuna aliyewajibu. Ilipofika saa sita mchana, Elia akaanza kuwadhihaki akisema, “Ombeni kwa sauti kubwa zaidi! Yeye ni mungu ati! Huenda ikawa amezama katika mawazo yake, amekwenda haja, au yumo safarini! Labda amelala, mnapaswa kumwamsha!” Manabii hao wakapiga kelele zaidi, wakajikatakata kwa visu na simi, kufuatana na desturi yao, hata wakabubujika damu. Wakaendelea kupiga makelele na kufanya kama wendawazimu hadi alasiri wakati wa kutoa tambiko; lakini hakuna aliyewajibu wala kuwajali. Basi, Elia akawaambia watu, “Sogeeni karibu nami.” Wao wakamkaribia. Kisha Elia akaijenga upya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu iliyokuwa imebomolewa. Alitwaa mawe kumi na mawili, hesabu ya makabila kumi na mawili yaliyopewa majina ya wana wa Yakobo ambaye Mwenyezi-Mungu alimwambia “Jina lako litakuwa Israeli.” Kwa mawe hayo, Elia alimjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu, akachimba na mtaro kuizunguka madhabahu hiyo; mtaro uwezao kuchukua kama debe moja na nusu la nafaka. Kisha akapanga kuni vizuri, akamkata vipandevipande yule fahali, akaviweka juu ya kuni. Kisha akawaambia watu, “Jazeni mitungi minne maji mkaimwagie tambiko hii ya kuteketezwa pamoja na kuni.” Wakafanya hivyo. Kisha akawaambia, “Rudieni tena.” Nao wakafanya hivyo mara ya pili. Naye akawaambia, “Fanyeni hivyo tena mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo. Maji yakatiririka chini pande zote za madhabahu, hata yakajaa mtaroni. Mnamo alasiri, wakati wa kutoa tambiko, nabii Elia aliikaribia madhabahu, akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, waoneshe watu leo hii kwamba wewe ndiwe Mungu wa Israeli, na kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya kwa amri yako. Unijibu, ee Mwenyezi-Mungu; unijibu ili watu hawa wajue kuwa wewe Mwenyezi-Mungu ndiwe Mungu, na kwamba umeigeuza mioyo yao wakurudie.” Mara, Mwenyezi-Mungu akashusha moto, ukaiteketeza tambiko hiyo ya kuteketezwa, kuni, mawe na vumbi, na kuyakausha maji yote mtaroni. Watu walipoona hivyo, walianguka kifudifudi na kusema, “Mwenyezi-Mungu, ni Mungu; Mwenyezi-Mungu, ni Mungu!” Ndipo Elia akawaambia, “Wakamateni manabii wote wa Baali. Msimwache hata mmoja wao atoroke!” Basi, watu wakawakamata wote, naye Elia akawapeleka mtoni Kishoni, akawaulia huko. Baada ya hayo, Elia akamwambia mfalme Ahabu, “Nenda ukale na kunywa. Nasikia kishindo cha mvua.” Basi, Ahabu akaenda zake kula na kunywa; naye Elia akapanda juu ya kilele cha mlima Karmeli, na huko akainama hadi chini na kuuweka uso wake katikati ya magoti yake. Kisha akamwambia mtumishi wake, “Sasa, nenda utazame upande wa baharini.” Mtumishi akaenda, akatazama, kisha akarudi akasema, “Hamna kitu.” Elia akamwambia, “Nenda tena mara saba.” Mara ya saba, huyo mtumishi akarudi, akasema, “Naona wingu dogo kama mkono wa mtu linatoka baharini.” Elia akamwambia, “Nenda umwambie mfalme Ahabu atayarishe gari lake la kukokotwa, ateremke, asije akazuiliwa na mvua.” Muda haukupita mrefu mbingu zikatanda mawingu mazito, upepo ukavuma, pakanyesha mvua kubwa. Ahabu naye akapanda gari lake la kukokotwa, akarudi Yezreeli. Nguvu ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Elia, naye akajifunga na kukaza joho lake, akakimbia na kumtangulia Ahabu kuingia mjini Yezreeli.
1 Wafalme 18:22-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa BWANA; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng’ombe wawili; wao na wajichagulie ng’ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng’ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la BWANA; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri. Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng’ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini. Wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya. Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe. Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika. Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia. Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la BWANA na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni. Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu. Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji. Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu, BWANA ndiye Mungu. Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko. Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele. Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba. Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie. Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli. Mkono wa BWANA ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuiingia Yezreeli.
1 Wafalme 18:22-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa BWANA; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkatakate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la BWANA; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri. Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng'ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini. Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakarukaruka juu ya madhabahu waliyoifanya. Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe. Wakapiga kelele, wakajikatakata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika. Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia. Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya makabila ya wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la BWANA na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng'ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni. Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu. Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji. Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Abrahamu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu, BWANA ndiye Mungu. Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko. Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele. Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Nenda tena mara saba. Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Nenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie. Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli. Mkono wa BWANA ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio akatangulia Ahabu mpaka kuiingia Yezreeli.
1 Wafalme 18:22-46 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha Eliya akawaambia, “Ni mimi peke yangu nabii wa BWANA aliyebaki, lakini Baali ana manabii mia nne na hamsini. Leteni mafahali wawili. Wao na wajichagulie mmoja, wamkate vipande vipande na waweke juu ya kuni lakini wasiiwashie moto. Nitamwandaa huyo fahali mwingine na kumweka juu ya kuni lakini sitawasha moto. Kisha mliitie jina la mungu wenu, nami nitaliitia jina la BWANA Mungu yule ambaye atajibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.” Kisha watu wote wakasema, “Hilo unalosema ni jema.” Eliya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni mmoja kati ya hawa mafahali na mwe wa kwanza kumwandaa, kwa kuwa ninyi mko wengi sana. Liitieni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.” Kwa hiyo wakamchukua yule fahali waliyepewa, nao wakamwandaa. Kisha wakaliitia jina la Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakapiga kelele, “Ee Baali, utujibu!” Lakini hapakuwa na jibu; hakuna aliyejibu. Nao wakacheza kuizunguka madhabahu waliyoijenga. Wakati wa adhuhuri, Eliya akaanza kuwadhihaki, akisema, “Pigeni kelele zaidi! Hakika yeye ni mungu! Labda amezama katika mawazo mazito, au ana shughuli nyingi, au amesafiri. Labda amelala usingizi mzito, naye ni lazima aamshwe.” Kwa hiyo wakapiga kelele zaidi na kama ilivyokuwa desturi yao wakajichanja wenyewe kwa visu na vyembe, mpaka damu ikachuruzika. Adhuhuri ikapita, nao wakaendelea na utabiri wao wa kiwazimu mpaka wakati wa dhabihu ya jioni. Lakini hapakuwa na jibu, hakuna aliyejibu, hakuna aliyeangalia. Kisha Eliya akawaambia watu wote, “Sogeeni karibu nami.” Watu wote wakamkaribia, naye akakarabati madhabahu ya BWANA, ambayo ilikuwa imevunjwa. Eliya akachukua mawe kumi na mawili, moja kwa ajili ya kila kabila la wana wa Yakobo, ambaye neno la BWANA lilimjia, likisema, “Jina lako litakuwa Israeli.” Kwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la BWANA, na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu. Akapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.” Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena. Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu. Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki. Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee BWANA, Mungu wa Abrahamu, na Isaki na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu katika Israeli na ya kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unijibu mimi, Ee BWANA, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee BWANA, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.” Kisha moto wa BWANA ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki. Wakati watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “BWANA: yeye ndiye Mungu! BWANA: yeye ndiye Mungu!” Kisha Eliya akawaamuru, “Wakamateni hao manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakawakamata, naye Eliya akawaleta mpaka Bonde la Kishoni na kuwachinja huko. Eliya akamwambia Ahabu, “Nenda, ukale na kunywa, kwa kuwa kuna sauti ya mvua kubwa.” Hivyo Ahabu akaondoka ili kula na kunywa. Lakini Eliya akapanda kileleni mwa Karmeli, akasujudu na akaweka kichwa chake katikati ya magoti yake. Akamwambia mtumishi wake, “Nenda ukatazame kuelekea bahari.” Akaenda na kutazama. Akasema, “Hakuna kitu chochote huko.” Mara saba Eliya akasema, “Nenda tena.” Mara ya saba, mtumishi akaleta taarifa, “Wingu dogo kama mkono wa mwanadamu linainuka kutoka baharini.” Hivyo Eliya akasema, “Nenda ukamwambie Ahabu, ‘Tandika gari lako na ushuke kabla mvua haijakuzuia.’ ” Wakati ule ule anga likawa jeusi kwa mawingu, upepo ukainuka na mvua kubwa ikanyesha, naye Ahabu akaenda zake Yezreeli. Nguvu za BWANA zikamjia Eliya, naye akajikaza viuno, akakimbia mbele ya Ahabu njia yote hadi maingilio ya Yezreeli.