Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Nya 29:21-30

1 Nya 29:21-30 SUV

Wakamtolea BWANA dhabihu, wakamchinjia BWANA sadaka za kuteketezwa, siku ya pili yake, yaani, ng’ombe elfu, na kondoo waume elfu, na wana-kondoo elfu, pamoja na sadaka zao za vinywaji, na dhabihu nyingi kwa ajili ya Israeli wote; wakala na kunywa mbele za BWANA siku ile, kwa furaha kuu. Wakamtawaza Sulemani, mwana wa Daudi, mara ya pili, wakamtia mafuta mbele za BWANA, awe mkuu, na Sadoki awe kuhani. Ndipo Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha BWANA, awe mfalme badala ya Daudi babaye, akafanikiwa; nao Israeli wote wakamtii. Nao wakuu wote, na mashujaa, na wana wote wa mfalme Daudi nao, wakajitia chini ya mfalme Sulemani. Naye BWANA akamtukuza Sulemani mno machoni pa Israeli wote, akampa fahari ya kifalme ya kumpita mfalme awaye yote aliyekuwa kabla yake katika Israeli. Basi Daudi, mwana wa Yese, akawa mfalme juu ya Israeli wote. Na wakati aliotawala juu ya Israeli, ulikuwa miaka arobaini; miaka saba alitawala Hebroni, na miaka thelathini na mitatu akatawala Yerusalemu. Akafa mwenye umri mwema, ameshiba siku, na mali, na heshima; naye Sulemani mwanawe akamiliki badala yake. Basi habari za mfalme Daudi, mwanzo na mwisho, angalia, zimeandikwa katika tarehe ya Samweli, mwonaji, na katika tarehe ya Nathani, nabii, na katika tarehe ya Gadi, mwonaji; pamoja na kutawala kwake kote na nguvu zake, nazo zamani zilizompata yeye, na Israeli, na falme zote za nchi.

Soma 1 Nya 29