1 Nyakati 29:21-30
1 Nyakati 29:21-30 NEN
Siku ya pili yake wakamtolea BWANA dhabihu na sadaka za kuteketezwa: mafahali 1,000, kondoo dume 1,000 na wana-kondoo dume 1,000, pamoja na sadaka za kinywaji na sadaka nyingine nyingi sana kwa ajili ya Israeli. Wakala na kunywa kwa furaha kubwa mbele za BWANA siku ile. Wakamtawaza Solomoni mwana wa Daudi mara ya pili kuwa mfalme, wakamtia mafuta kwa ajili ya BWANA ili awe mfalme na Sadoki kuwa kuhani. Solomoni akaketi kwenye kiti cha enzi cha BWANA kuwa mfalme mahali pa Daudi baba yake. Akafanikiwa sana na Israeli wote wakamtii. Maafisa wote na mashujaa, pamoja na wana wote wa Daudi, wakaahidi kumtii Mfalme Solomoni. BWANA akamtukuza sana Solomoni mbele ya Israeli wote na kumvika fahari ya kifalme ambayo hakuna mfalme yeyote wa Israeli kabla yake aliwahi kuwa nayo. Daudi mwana wa Yese alikuwa mfalme wa Israeli yote. Alitawala Israeli kwa miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu. Daudi akafa akiwa mzee mwenye umri mwema, akiwa ameshiba siku, utajiri na heshima. Naye Solomoni mwanawe akawa mfalme baada yake. Kuhusu matukio ya utawala wa Mfalme Daudi, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kumbukumbu za mwonaji Samweli, na kumbukumbu za nabii Nathani na kumbukumbu za mwonaji Gadi, pamoja na habari zote za utawala wake, nguvu zake na matukio yaliyompata yeye, na Israeli, na falme za nchi nyingine zote.