Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Sefania 1

1
1Neno la Mwenyezi Mungu lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda:
Onyo la maangamizi yanayokuja
2Mwenyezi Mungu asema,
“Nitafagia kila kitu
kutoka uso wa dunia.
3Nitafagilia mbali watu na wanyama;
nitafagilia mbali ndege wa angani
na samaki wa baharini.
Wafanyao maovu watapata tu kokoto,
nami nitamkatilia mbali mwanadamu atoke katika dunia,”
asema Mwenyezi Mungu.
Dhidi ya Yuda
4“Nitaiadhibu Yuda
na wote wanaoishi Yerusalemu.
Kutoka mahali hapa nitakatilia mbali
kila mabaki ya Baali,
majina ya wapagani na makuhani
waabuduo sanamu:
5wale ambao husujudu juu ya mapaa
kuabudu jeshi la vitu vya angani,
wale ambao husujudu na kuapa kwa Mwenyezi Mungu
na ambao pia huapa kwa Malkamu,
6wale wanaoacha kumfuata Mwenyezi Mungu,
wala hawamtafuti Mwenyezi Mungu
wala kutaka shauri lake.
7Nyamazeni mbele za Bwana Mungu Mwenyezi,
kwa maana siku ya Mwenyezi Mungu iko karibu.
Mwenyezi Mungu ameandaa dhabihu,
amewaweka wakfu wale aliowaalika.
8Katika siku ya dhabihu ya Mwenyezi Mungu
nitawaadhibu wakuu
na wana wa mfalme
na wale wote wanaovaa
nguo za kigeni.
9Katika siku hiyo nitaadhibu wote ambao
hukwepa kukanyaga kizingiti,
ambao hujaza hekalu la miungu yao
kwa dhuluma na udanganyifu.”
10Mwenyezi Mungu asema, “Katika siku hiyo
kilio kitapanda juu kutoka lango la Samaki,
maombolezo kutoka mtaa wa pili,
na mshindo mkubwa kutoka vilimani.
11Ombolezeni, ninyi mnaoishi katika eneo la sokoni;
wafanyabiashara wenu wote wameangamizwa,
wote ambao wanafanya biashara ya fedha
wataangamizwa.
12Wakati huo nitaupekua mji wa Yerusalemu kwa taa,
na kuwaadhibu wale ambao
wanakaa katika hali ya kuridhika,
ambao ni kama divai
iliyobaki kwenye machicha,
ambao hudhani, ‘Mwenyezi Mungu hatafanya lolote,
jema au baya.’
13Utajiri wao utatekwa nyara,
nyumba zao zitabomolewa.
Watajenga nyumba,
lakini hawataishi ndani yake;
watapanda mizabibu
lakini hawatakunywa divai yake.
Siku kubwa ya Mwenyezi Mungu
14“Siku kubwa ya Mwenyezi Mungu iko karibu:
iko karibu na inakuja haraka.
Sikilizeni! Kilio katika siku ya Mwenyezi Mungu
kitakuwa chungu.
Shujaa atapiga ukelele wa vita huko.
15Siku ile ni siku ya ghadhabu,
siku ya fadhaa na dhiki,
siku ya uharibifu na ukiwa,
siku ya giza na utusitusi,
siku ya mawingu na giza nene,
16siku ya tarumbeta na kelele za vita
dhidi ya miji yenye ngome,
na dhidi ya minara mirefu.
17Nitawaletea watu dhiki,
nao watatembea kama vipofu,
kwa sababu wametenda dhambi
dhidi ya Mwenyezi Mungu.
Damu yao itamwagwa kama vumbi
na matumbo yao kama kinyesi.
18Fedha yao wala dhahabu yao
hazitaweza kuwaokoa
katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.
Katika moto wa wivu wake
dunia yote itateketezwa,
kwa maana ghafula ataleta mwisho
wa wote wanaoishi duniani.”

Iliyochaguliwa sasa

Sefania 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia