Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 5

5
Matokeo ya kuhesabiwa haki
1Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kupitia kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi, 2ambaye kupitia kwake tumepata kuifikia neema hii kupitia kwa imani, neema ambayo tunasimama ndani yake sasa. Nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kupitia kwa Roho wa Mungu ambaye ametupatia.
6Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Al-Masihi alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Al-Masihi alikufa kwa ajili yetu.
9Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kupitia kwa kifo cha Mwanawe, si zaidi sana baada ya kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kupitia kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.
Adamu alileta kifo, Isa ameleta uzima
12Kwa hiyo kama vile dhambi ilivyoingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja, na kupitia dhambi hii mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote wamefanya dhambi: 13kwa maana kabla sheria haijatolewa, dhambi ilikuwemo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi wakati hakuna sheria. 14Hata hivyo, tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Musa, mauti ilitawala watu wote, hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa kuvunja amri, kama alivyofanya Adamu, aliye mfano wa yule atakayekuja.
15Lakini ile karama iliyotolewa haikuwa kama lile kosa. Kwa maana ikiwa watu wengi walikufa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja, basi neema ya Mungu na ile karama iliyokuja kwa neema ya mtu mmoja, yaani Isa Al-Masihi, imezidi kuwa nyingi kwa ajili ya wengi. 16Tena ile karama ya Mungu haiwezi kulinganishwa na matokeo ya ile dhambi ya mtu mmoja. Kwani hukumu ilikuja kupitia kwa dhambi ya mtu mmoja, ikaleta adhabu; lakini ile karama ilikuja baada ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. 17Kwa maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kupitia kwa huyo mtu mmoja, yaani Isa Al-Masihi.
18Kwa hiyo, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta adhabu kwa watu wote, vivyo hivyo pia kwa tendo la haki la mtu mmoja lilileta kuhesabiwa haki ambako huleta uzima kwa wote. 19Kwa maana kama vile kupitia kutokutii kwa yule mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kupitia kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki.
20Zaidi ya hayo, sheria ilikuja, ili uvunjaji wa sheria uongezeke. Lakini dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi, 21ili kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo neema iweze kutawala kupitia kwa haki hata kuleta uzima wa milele katika Isa Al-Masihi Bwana wetu.

Iliyochaguliwa sasa

Warumi 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia