Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 4

4
Ibrahimu alihesabiwa haki kwa imani
1Tuseme nini basi, kuhusu Ibrahimu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili? 2Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu. 3Kwa maana Maandiko yasemaje? “Ibrahimu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”#4:3 Mwanzo 15:6
4Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili. 5Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki. 6Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena kuhusu baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo:
7“Wamebarikiwa wale
ambao wamesamehewa makosa yao,
ambao dhambi zao zimefunikwa.
8Heri mtu yule
Mwenyezi Mungu hamhesabii dhambi zake.”#4:8 Zaburi 32:1, 2
Haki kabla ya tohara
9Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tumesema imani ya Ibrahimu ilihesabiwa kwake kuwa haki. 10Je, ilihesabiwaje kwake kuwa haki? Ni kabla ya kutahiriwa, au baada yake kutahiriwa? Haikuwa baada yake kutahiriwa, bali kabla hajatahiriwa! 11Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote waaminio pasipo kutahiriwa, ili wahesabiwe kuwa wenye haki. 12Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo baba yetu Ibrahimu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.
Ahadi ya Mwenyezi Mungu hufahamika kwa imani
13Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Ibrahimu au kwa wazao wake kupitia kwa sheria bali kupitia kwa haki ipatikanayo kwa imani. 14Kwa maana ikiwa wale wanaoishi kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, 15kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria, hakuna makosa.
16Kwa hiyo, ahadi huja kupitia kwa imani, ili iwe ni kwa neema, na ihakikishiwe wazao wote wa Ibrahimu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Ibrahimu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote. 17Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.”#4:17 Mwanzo 17:5 Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anayefufua waliokufa, na kuvitaja vitu ambavyo haviko kana kwamba viko.
Mfano wa imani ya Ibrahimu
18Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Ibrahimu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”#4:18 Mwanzo 15:5 19Ibrahimu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri hali ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri hali ya kufa ya tumbo la Sara. 20Lakini Ibrahimu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, 21akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi. 22Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.”#4:22 Mwanzo 15:6 23Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake, 24bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupatia haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Isa Bwana wetu kutoka kwa wafu. 25Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.

Iliyochaguliwa sasa

Warumi 4: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia