Warumi 5:12-19
Warumi 5:12-19 NENO
Kwa hiyo kama vile dhambi ilivyoingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja, na kupitia dhambi hii mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote wamefanya dhambi: kwa maana kabla sheria haijatolewa, dhambi ilikuwemo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi wakati hakuna sheria. Hata hivyo, tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Musa, mauti ilitawala watu wote, hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa kuvunja amri, kama alivyofanya Adamu, aliye mfano wa yule atakayekuja. Lakini ile karama iliyotolewa haikuwa kama lile kosa. Kwa maana ikiwa watu wengi walikufa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja, basi neema ya Mungu na ile karama iliyokuja kwa neema ya mtu mmoja, yaani Isa Al-Masihi, imezidi kuwa nyingi kwa ajili ya wengi. Tena ile karama ya Mungu haiwezi kulinganishwa na matokeo ya ile dhambi ya mtu mmoja. Kwani hukumu ilikuja kupitia kwa dhambi ya mtu mmoja, ikaleta adhabu; lakini ile karama ilikuja baada ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. Kwa maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kupitia kwa huyo mtu mmoja, yaani Isa Al-Masihi. Kwa hiyo, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta adhabu kwa watu wote, vivyo hivyo pia kwa tendo la haki la mtu mmoja lilileta kuhesabiwa haki ambako huleta uzima kwa wote. Kwa maana kama vile kupitia kutokutii kwa yule mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kupitia kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki.