Warumi 4:9-15
Warumi 4:9-15 NEN
Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki.” Je, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa. Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki. Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani. Kwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa.