Waroma 4:9-15
Waroma 4:9-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: “Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.” Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa, ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa. Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu. Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa. Mungu alimwahidi Abrahamu na wazawa wake kwamba ulimwengu ungekuwa mali yao. Ahadi hiyo haikufanywa kwa sababu Abrahamu aliitii sheria, bali kwa kuwa aliamini, akakubaliwa kuwa mwadilifu. Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu wanaoitii sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu. Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna sheria, haiwezekani kuivunja.
Waroma 4:9-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi je! Heri hiyo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa tunanena ya kwamba kwake Abrahamu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki. Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa. Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, mhuri wa ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki; tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Abrahamu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa. Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Abrahamu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani. Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika. Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa.
Waroma 4:9-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi je! Uheri huo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa twanena ya kwamba kwake Ibrahimu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki. Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa. Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, muhuri ya ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki; tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Ibrahimu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa. Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani. Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika. Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa.
Waroma 4:9-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki.” Je, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa. Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki. Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani. Kwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa.