Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 2

2
Hukumu ya Mwenyezi Mungu
1Kwa hiyo huna udhuru wowote, wewe utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana katika jambo lolote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo hayo hayo. 2Basi tunajua kwamba hukumu ya Mungu dhidi ya wale wafanyao mambo kama hayo ni ya kweli. 3Hivyo wewe mwanadamu, unapotoa hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu? 4Au waudharau wingi wa wema, ustahimili na uvumilivu wake, bila kujua kuwa wema wa Mungu wakuelekeza kwenye toba?
5Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa. 6Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu kulingana na matendo yake#2:6 Zaburi 62:12; Mithali 24:12. 7Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. 8Lakini kwa wale wanaotafuta mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia, 10bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa. 11Kwa maana Mungu hana upendeleo.
12Watu wote waliotenda dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria, nao wote waliotenda dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria. 13Kwa maana si wale wanaoisikia sheria ambao ni wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale wanaoitii sheria ndio watakaohesabiwa haki. 14(Naam, wakati wa watu wa Mataifa, ambao hawana sheria, wanapofanya kwa asili mambo yatakiwayo na sheria, wao ni sheria kwa nafsi zao wenyewe, hata ingawa hawana sheria. 15Wao wanaonesha kwamba lile linalotakiwa na sheria limeandikwa kwenye mioyo yao, ambayo pia dhamiri zao zikiwashuhudia, nayo mawazo yao yenye kupingana yatawashtaki au kuwatetea.) 16Hili litatukia siku hiyo Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu kupitia kwa Isa Al-Masihi, kama isemavyo Injili yangu.
Wayahudi na Torati
17Tazama, wewe ukiwa unajiita Myahudi na kuitegemea Torati na kujisifia uhusiano wako na Mungu, 18kama unajua mapenzi ya Mungu na kukubali lililo bora kwa sababu umefundishwa na hiyo Torati, 19kama unatambua kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, na mwanga kwa wale walio gizani, 20mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una maarifa ya kweli katika hiyo Torati, 21basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba? 22Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu? 23Wewe ujivuniaye Torati, wamwaibisha Mungu kwa kuvunja Torati? 24Kama ilivyoandikwa, “Kwa ajili yenu ninyi, Jina la Mungu linatukanwa miongoni mwa watu wa Mataifa.”#2:24 Isaya 52:5; Ezekieli 36:22
25Kutahiriwa kuna thamani ikiwa unatii Torati, lakini kama unavunja Torati, kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. 26Hivyo, ikiwa wale wasiotahiriwa wanatimiza mambo ambayo Torati inataka, je, kutokutahiriwa kwao hakutahesabiwa kuwa sawa na kutahiriwa? 27Ndipo wale ambao hawakutahiriwa kimwili lakini wanaitii Torati watawahukumu ninyi, ambao ingawa mmetahiriwa na kuijua sana Torati ya Mungu iliyoandikwa, lakini mwaivunja.
28Kwa maana mtu si Myahudi kwa vile alivyo kwa nje, wala tohara ya kweli si kitu cha nje au cha kimwili. 29Lakini mtu ni Myahudi alivyo ndani, nayo tohara ya kweli ni jambo la moyoni, ni la Roho wa Mungu, wala si la sheria iliyoandikwa. Mtu kama huyo hapokei sifa kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu.

Iliyochaguliwa sasa

Warumi 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia