Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 1

1
Salamu
1Paulo, mtumishi wa Al-Masihi Isa, aliyeitwa kuwa mtume na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu, 2Injili ambayo Mungu alitangulia kuiahidi kwa vinywa vya manabii wake katika Maandiko Matakatifu, 3yaani Injili inayomhusu Mwanawe, yeye ambaye kwa uzao wa mwili alikuwa mzao wa Daudi, 4na ambaye kwa uwezo wa Roho wa utakatifu alidhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu#1:4 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili. kwa ufufuo wake kutoka kwa wafu, yaani Isa Al-Masihi, Bwana wetu. 5Kupitia kwake tumepokea neema na utume ili kuwaita watu wote wa mataifa waje kwenye utii utokanao na imani kwa ajili ya jina lake. 6Ninyi nyote pia mko miongoni mwa watu walioitwa ili wapate kuwa mali ya Isa Al-Masihi.
7Kwa wote walio Rumi wanaopendwa na Mungu na kuitwa kuwa watakatifu.
Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba#1:7 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
Maombi na shukrani
8Kwanza kabisa, namshukuru Mungu wangu kupitia kwa Isa Al-Masihi kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inatangazwa duniani kote. 9Kwa maana Mungu ninayemtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Injili ya Mwanawe, ni shahidi wangu jinsi ninavyowakumbuka daima 10katika maombi yangu siku zote. Nami ninaomba kwamba hatimaye sasa kwa mapenzi ya Mungu, njia ipate kufunguliwa kwa ajili yangu ili nije kwenu.
11Ninatamani sana kuwaona ili nipate kuwapa karama za rohoni ili mwe imara, 12au zaidi, ninyi pamoja nami tuweze kutiana moyo katika imani sisi kwa sisi. 13Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mara nyingi nimekusudia kuja kwenu (ingawa hadi sasa nimezuiliwa), ili nipate kuvuna mavuno miongoni mwenu kama nilivyovuna miongoni mwa watu wa Mataifa wengine.
14Mimi ni mdeni kwa Wayunani na kwa wasio Wayunani, kwa wenye hekima na kwa wasio na hekima. 15Ndiyo sababu ninatamani sana kuihubiri Injili kwenu pia ninyi mlioko Rumi.
16Mimi siionei haya Injili, kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia. 17Kwa maana katika Injili haki ya Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”#1:17 Habakuki 2:4
Ghadhabu ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu
18Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao. 19Kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani uweza wake wa milele na asili yake ya uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.
21Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga, 23na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizotengenezwa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vinavyotambaa.
24Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakaivunjia heshima miili yao wao kwa wao. 25Waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.
26Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wazifuate tamaa za aibu. Hata wanawake wao wakabadili mahusiano ya kimwili ya asili kwa mahusiano yasiyokusudiwa. 27Vivyo hivyo wanaume pia wakaacha mahusiano ya kimwili ya asili na wanawake, wakawakiana kwa tamaa mbaya wao kwa wao. Wanaume wakafanya matendo ya aibu na wanaume wengine, nao wakapata adhabu waliyostahili kwa ajili ya upotovu wao.
28Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. 29Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, 30wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, 31wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. 32Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.

Iliyochaguliwa sasa

Warumi 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia