Warumi 14
14
Msiwahukumu wengine
1Mkaribisheni yeye ambaye imani yake ni dhaifu, lakini si kwa kugombana na kubishana juu ya mawazo yake. 2Mtu mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu, lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula mboga tu. 3Yeye alaye kila kitu asimdharau yeye asiyekula. Wala yeye asiyekula kila kitu asimhukumu yule alaye kila kitu, kwa maana Mungu amemkubali. 4Wewe ni nani hata umhukumu mtumishi wa mtu mwingine? Kwa bwana wake tu anasimama au kuanguka. Naye atasimama kwa sababu Bwana anaweza kumsimamisha.
5Mtu mmoja anaitukuza siku fulani kuwa ni bora kuliko nyingine, na mwingine anaona kuwa siku zote ni sawa. Basi kila mmoja awe na hakika na yale anayoamini. 6Yeye anayehesabu siku moja kuwa takatifu kuliko nyingine, hufanya hivyo kwa kumheshimu Mwenyezi Mungu. Naye alaye nyama hula kwa Mwenyezi Mungu, kwa maana humshukuru Mungu, naye akataaye kula nyama hufanya hivyo kwa Mwenyezi Mungu na humshukuru Mungu. 7Kwa kuwa hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna hata mmoja wetu afaye kwa ajili yake mwenyewe. 8Kama tunaishi, tunaishi kwa Mwenyezi Mungu, nasi pia tukifa tunakufa kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo basi, kama tukiishi au kama tukifa, sisi ni mali ya Mwenyezi Mungu.
9Kwani kwa sababu hii hasa, Al-Masihi alikufa na akawa hai tena kusudi apate kuwa Bwana wa wote, yaani waliokufa na walio hai.
10Basi kwa nini wewe wamhukumu ndugu yako? Au kwa nini wewe unamdharau ndugu yako? Kwa kuwa sote tutasimama mbele ya kiti cha Mungu cha hukumu. 11Kwa kuwa imeandikwa:
“ ‘Kama vile niishivyo,’#14:11 Isaya 45:23 asema Mwenyezi Mungu,
‘kila goti litapigwa mbele zangu,
na kila ulimi utakiri kwa Mungu.’ ”
12Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu.
Usimfanye ndugu Yako ajikwae
13Kwa hiyo tusiendelee kuhukumiana. Badala yake mtu aamue kutoweka kamwe kikwazo au kizuizi katika njia ya ndugu mwingine. 14Ninajua tena nimehakikishiwa sana katika Bwana Isa kwamba hakuna kitu chochote ambacho ni najisi kwa asili yake. Lakini kama mtu anakiona kitu kuwa ni najisi, basi kwake huyo kitu hicho ni najisi. 15Kama ndugu yako anahuzunishwa kwa sababu ya kile unachokula, basi huenendi tena katika upendo. Usiruhusu kile unachokula kiwe sababu ya kumwangamiza ndugu yako ambaye Al-Masihi alikufa kwa ajili yake. 16Usiruhusu kile ambacho unakiona kuwa chema kisemwe kuwa ni kiovu. 17Kwa maana ufalme wa Mungu si kula na kunywa, bali ni haki, amani na furaha katika Roho wa Mungu. 18Kwa sababu mtu yeyote anayemtumikia Al-Masihi kwa jinsi hii, anampendeza Mungu na kukubaliwa na wanadamu.
19Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi. 20Usiiharibu kazi ya Mungu kwa ajili ya chakula. Hakika vyakula vyote ni safi, lakini ni kosa kula kitu chochote kinachomsababisha ndugu yako ajikwae. 21Ni afadhali kutokula nyama wala kunywa divai au kufanya jambo lingine lolote litakalomsababisha ndugu yako ajikwae.
22Je, wewe unayo imani? Ile imani uliyo nayo, uwe nayo nafsini mwako mbele za Mungu. Heri mtu yule asiye na sababu ya kujihukumu nafsi yake kwa ajili ya kile anachokifanya. 23Lakini kama mtu ana shaka kuhusu kile anachokula, amehukumiwa, kwa sababu hakula kwa imani. Kwa kuwa chochote kinachofanywa pasipo imani ni dhambi.
Iliyochaguliwa sasa
Warumi 14: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.