Zaburi 91:1-16
Zaburi 91:1-16 NENO
Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana, atadumu katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema kumhusu Mwenyezi Mungu, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu, ninayemtumaini.” Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji, na maradhi ya kuambukiza ya kuua. Atakufunika kwa manyoya yake, chini ya mabawa yake utapata kimbilio, uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako. Hutaogopa vitisho vya usiku, wala mshale urukao mchana, wala maradhi ya kuambukiza yanayonyemelea gizani, wala tauni iharibuyo adhuhuri. Ijapo watu elfu wataangukia kando yako, kumi elfu mkono wako wa kuume, lakini haitakukaribia wewe. Utatazama tu kwa macho yako na kuona adhabu ya waovu. Ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako; naam, Mwenyezi Mungu ambaye ni kimbilio langu; basi hakuna madhara yatakayokupata wewe, hakuna maafa yatalikaribia hema lako. Kwa kuwa atawaagiza malaika wake kwa ajili yako, wakulinde katika njia zako zote. Watakuchukua mikononi mwao, ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka wakali, simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu. Mwenyezi Mungu asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa; nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu. Ataniita, nami nitamjibu; nitakuwa pamoja naye katika taabu, nitamwokoa na kumheshimu. Kwa siku nyingi nitamshibisha na kumwonesha wokovu wangu.”