Zaburi 91:1-16
Zaburi 91:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!” Hakika Mungu atakuokoa katika mtego; atakukinga na maradhi mabaya. Atakufunika kwa mabawa yake, utapata usalama kwake; mkono wake utakulinda na kukukinga. Huna haja ya kuogopa vitisho vya usiku, wala shambulio la ghafla mchana; huna haja ya kuogopa baa lizukalo usiku, wala maafa yanayotokea mchana. Hata watu elfu wakianguka karibu nawe, naam, elfu kumi kuliani mwako, lakini wewe baa halitakukaribia. Kwa macho yako mwenyewe utaangalia, na kuona jinsi watu waovu wanavyoadhibiwa. Wewe umemfanya Mwenyezi-Mungu kuwa kimbilio lako; naam, Mungu aliye juu kuwa kinga yako. Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.”
Zaburi 91:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Aketiye mahali pa siri pake Aliye Juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Atasema, BWANA ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Maana Yeye atakuokoa kutoka kwa mtego wa mwindaji, Na katika maradhi mabaya. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Hutaogopa hatari za usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala mapigo yajayo usiku, Wala maafa yatokeayo adhuhuri, Hata watu elfu wakianguka ubavuni pako. Naam, watu elfu kumi katika mkono wako wa kulia! Wewe hutakaribiwa na maafa. Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki. Kwa kuwa Wewe BWANA ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye Juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika wake Wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka, Mwanasimba na joka utawakanyaga kwa miguu. Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu. Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza; Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonesha wokovu wangu.
Zaburi 91:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, BWANA ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri, Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe. Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki. Kwa kuwa Wewe BWANA ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu. Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu. Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza; Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu.
Zaburi 91:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana, atadumu katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema kumhusu BWANA, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.” Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji, na maradhi ya kuambukiza ya kuua. Atakufunika kwa manyoya yake, chini ya mbawa zake utapata kimbilio, uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako. Hutaogopa vitisho vya usiku, wala mshale urukao mchana, wala maradhi ya kuambukiza yanayonyemelea gizani, wala tauni iharibuyo adhuhuri. Ijapo watu elfu wataangukia kando yako, kumi elfu mkono wako wa kuume, lakini haitakukaribia wewe. Utatazama tu kwa macho yako na kuona adhabu ya waovu. Kama ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako: naam, BWANA ambaye ni kimbilio langu, basi hakuna madhara yatakayokupata wewe, hakuna maafa yataikaribia hema yako. Kwa kuwa atawaagiza malaika zake kwa ajili yako, wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuinua, ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka wakali, simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu. BWANA asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa; nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu. Ataniita, nami nitamjibu; nitakuwa pamoja naye katika taabu, nitamwokoa na kumheshimu. Kwa siku nyingi nitamshibisha na kumwonyesha wokovu wangu.”