Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 90

90
Kitabu cha Nne
(Zaburi 90–106)
Zaburi 90
Umilele wa Mwenyezi Mungu na udhaifu wa mwanadamu
Maombi ya Musa, mtu wa Mungu.
1Bwana, wewe umekuwa makao yetu
katika vizazi vyote.
2Kabla ya kuzaliwa milima
au hujaumba dunia na ulimwengu,
wewe ni Mungu tangu milele hata milele.
3Huwarudisha watu mavumbini,
ukisema, “Rudini mavumbini, enyi wanadamu.”
4Kwa maana kwako miaka elfu
ni kama siku moja iliyokwisha pita,
au kama kesha la usiku.
5Unawatowesha wanadamu katika usingizi wa kifo,
nao ni kama majani machanga ya asubuhi:
6ingawa asubuhi yanachipua,
ifikapo jioni huwa yamenyauka na kukauka.
7Tumeangamizwa kwa hasira yako
na tumetishwa kwa ghadhabu yako.
8Umeyaweka maovu yetu mbele yako,
dhambi zetu za siri katika nuru ya uwepo wako.
9Tumeishi siku zetu zote chini ya ghadhabu yako,
tunamaliza miaka yetu kwa kuomboleza.
10Siku zetu za kuishi ni miaka sabini,
au miaka themanini ikiwa tuna nguvu,
lakini yote ni ya shida na taabu,
nazo zapita haraka, nasi twatoweka.
11Ni nani ajuaye nguvu za hasira yako?
Kwa maana ghadhabu yako ni kubwa
kama hofu tunayopaswa kuwa nayo kwako.
12Tufundishe kuzihesabu siku zetu vizuri,
ili tujipatie moyo wa hekima.
13Ee Mwenyezi Mungu, uwe na huruma! Utakawia hata lini?
Wahurumie watumishi wako.
14Tushibishe asubuhi kwa upendo wako usiokoma,
ili tuweze kuimba kwa shangwe na kufurahi siku zetu zote.
15Utufurahishe kulingana na siku ulizotuadhibu,
kulingana na miaka tuliyotaabika.
16Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako,
utukufu wako kwa watoto wao.
17Wema wa Bwana Mungu wetu uwe juu yetu;
uzithibitishe kazi za mikono yetu:
naam, uzithibitishe kazi za mikono yetu.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 90: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia