Zaburi 51:10-19
Zaburi 51:10-19 NEN
Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu. Usinitupe kutoka mbele zako wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu. Unirudishie tena furaha ya wokovu wako, unipe roho ya utii, ili initegemeze. Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako, na wenye dhambi watakugeukia wewe. Ee Mungu, Mungu uniokoaye, niokoe na hatia ya kumwaga damu, nao ulimi wangu utaimba juu ya haki yako. Ee BWANA, fungua midomo yangu, na kinywa changu kitatangaza sifa zako. Wewe hupendezwi na dhabihu, au ningaliileta, hufurahii sadaka za kuteketezwa. Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika, moyo uliovunjika wenye toba, Ee Mungu, hutaudharau. Kwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi, ukazijenge upya kuta za Yerusalemu. Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki, sadaka nzima za kuteketezwa za kukupendeza sana, pia mafahali watatolewa madhabahuni mwako.