Zaburi 51:10-19
Zaburi 51:10-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Uniumbie moyo safi, ee Mungu, uweke ndani yangu roho mpya na thabiti. Usinitupe mbali nawe; usiniondolee roho yako takatifu. Unifanye nifurahi tena kwa kuniokoa, utegemeze ndani yangu moyo wa utii. Hapo nitawafunza wakosefu njia yako, nao wenye dhambi watarudi kwako. Uniokoe na hatia ya umwagaji damu, ee Mungu, Mungu mwokozi wangu, nami nitaimba kwa sauti kuwa umeniokoa. Uniwezeshe kusema, ee Bwana, midomo yangu itangaze sifa zako. Kwa kweli wewe hupendezwi na tambiko, ama sivyo mimi ningalikutolea. Wewe huna haja na tambiko za kuteketezwa. tambiko yangu kwako ee Mungu, ni moyo mnyofu; wewe, ee Mungu, hukatai moyo mnyofu na mtiifu. Ee Mungu, upende kuutendea mema mji wa Siyoni; uzijenge tena upya kuta za mji wa Yerusalemu. Hapo utapendezwa na tambiko za kweli: Sadaka za kuteketezwa na za kuteketezwa nzima; mafahali watatolewa tambiko madhabahuni pako.
Zaburi 51:10-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya na kuithibiti roho yangu. Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya upendo. Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako. Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na umwagaji wa damu, Na ulimi wangu utaiimba haki yako. Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako. Maana hupendezwi na dhabihu, na kama ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako, Uzijenge kuta za Yerusalemu. Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki, Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. Ndipo watakapotoa ng'ombe Juu ya madhabahu yako.
Zaburi 51:10-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi. Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako. Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na damu za watu, Na ulimi wangu utaiimba haki yako. Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako, Uzijenge kuta za Yerusalemu. Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki, Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. Ndipo watakapotoa ng’ombe Juu ya madhabahu yako.
Zaburi 51:10-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu. Usinitupe kutoka mbele zako wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu. Unirudishie tena furaha ya wokovu wako, unipe roho ya utii, ili initegemeze. Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako, na wenye dhambi watakugeukia wewe. Ee Mungu, Mungu uniokoaye, niokoe na hatia ya kumwaga damu, nao ulimi wangu utaimba juu ya haki yako. Ee BWANA, fungua midomo yangu, na kinywa changu kitatangaza sifa zako. Wewe hupendezwi na dhabihu, au ningaliileta, hufurahii sadaka za kuteketezwa. Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika, moyo uliovunjika wenye toba, Ee Mungu, hutaudharau. Kwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi, ukazijenge upya kuta za Yerusalemu. Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki, sadaka nzima za kuteketezwa za kukupendeza sana, pia mafahali watatolewa madhabahuni mwako.