Zaburi 26:1-12
Zaburi 26:1-12 NENO
Ee Mwenyezi Mungu, nithibitishe katika haki, maana nimeishi maisha yasiyo na lawama; nimemtumainia Mwenyezi Mungu bila kusitasita. Ee Mwenyezi Mungu, unijaribu, unipime, uuchunguze moyo wangu na mawazo yangu; kwa maana upendo wako uko mbele yangu daima, nami natembea siku zote katika kweli yako. Siketi pamoja na watu wadanganyifu, wala siandamani na wanafiki, ninachukia kusanyiko la watenda maovu, na ninakataa kuketi pamoja na waovu. Ninanawa mikono yangu kwa kuwa sina hatia, naikaribia madhabahu yako, Ee Mwenyezi Mungu, nikitangaza sifa yako kwa sauti kubwa, huku nikisimulia matendo yako ya ajabu. Ee Mwenyezi Mungu, naipenda nyumba yako unakoishi, mahali pale utukufu wako hukaa. Usiiondoe nafsi yangu pamoja na watenda dhambi, wala uhai wangu pamoja na wanaomwaga damu, ambao mikononi mwao kuna mipango miovu, ambao mikono yao ya kuume imejaa rushwa. Bali mimi ninaishi maisha yasiyo na lawama; nikomboe na unihurumie. Miguu yangu imesimama katika uwanja tambarare; katika kusanyiko kuu nitamsifu Mwenyezi Mungu.