Zaburi 22:1-19
Zaburi 22:1-19 NEN
Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa? Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu, hata usiku, sinyamazi. Hata hivyo umesimikwa katika kiti cha enzi kama Uliye Mtakatifu; wewe ni sifa ya Israeli. Kwako wewe baba zetu waliweka tumaini lao, walikutumaini nawe ukawaokoa. Walikulilia wewe na ukawaokoa, walikutegemea wewe nao hawakuaibika. Mimi ni mnyoo wala si mwanadamu, wanaume wamenibeza, na watu wamenidharau. Wote wanionao hunidhihaki, hunivurumishia matusi, wakitikisa vichwa vyao: Husema, “Anamtegemea BWANA, basi BWANA na amwokoe. Amkomboe basi, kwa maana anapendezwa naye.” Hata hivyo ulinitoa tumboni, ukanifanya nikutegemee, hata nilipokuwa ninanyonya matiti ya mama yangu. Nimekabidhiwa kwako tangu kuzaliwa, toka tumboni mwa mama yangu umekuwa Mungu wangu. Usiwe mbali nami, kwa maana shida iko karibu na hakuna wa kunisaidia. Mafahali wengi wamenizunguka, mafahali wa Bashani wenye nguvu wamenizingira. Simba wangurumao wanaorarua mawindo yao hupanua vinywa vyao dhidi yangu. Nimemiminwa kama maji, mifupa yangu yote imetoka katika viungo vyake. Moyo wangu umegeuka kuwa nta, umeyeyuka ndani yangu. Nguvu zangu zimekauka kama kigae, ulimi wangu umegandamana na kaakaa la kinywa changu, kwa sababu umenilaza katika mavumbi ya kifo. Mbwa wamenizunguka, kundi la watu waovu limenizingira, wametoboa mikono yangu na miguu yangu. Naweza kuhesabu mifupa yangu yote, watu wananikodolea macho na kunisimanga. Wanagawana nguo zangu wao kwa wao, na vazi langu wanalipigia kura. Lakini wewe, Ee BWANA, usiwe mbali. Ee Nguvu yangu, uje haraka unisaidie.