Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 17:1-15

Zaburi 17:1-15 NENO

Sikia, Ee Mwenyezi Mungu, kusihi kwangu kwa haki, sikiliza kilio changu. Tega sikio kwa ombi langu, halitoki katika midomo ya udanganyifu. Hukumu yangu na itoke kwako, macho yako na yaone yale yaliyo haki. Ingawa unauchunguza moyo wangu na kunikagua usiku, ingawa umenijaribu, hutaona chochote. Nimeamua kwamba kinywa changu hakitatenda dhambi. Kuhusu matendo ya wanadamu: kwa neno la midomo yako, nimejiepusha na njia za wenye jeuri. Hatua zangu zimeshikamana na njia zako; nyayo zangu hazikuteleza. Ee Mungu, ninakuita, kwa kuwa utanijibu, nitegee sikio lako na usikie ombi langu. Uoneshe ajabu ya upendo wako mkuu, wewe unayeokoa kwa mkono wako wa kuume wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao. Nilinde kama mboni ya jicho lako, unifiche chini ya kivuli cha mabawa yako kutokana na waovu wanaonishambulia, kutokana na adui wauaji wanaonizunguka. Huifunga mioyo yao iliyo migumu, vinywa vyao hunena kwa majivuno. Wamenifuatia nyayo zangu, sasa wamenizingira, wakiwa macho, waniangushe chini. Wamefanana na simba mwenye njaa anayewinda, kama simba mkubwa anayenyemelea mafichoni. Inuka, Ee Mwenyezi Mungu, pambana nao, uwaangushe, niokoe kwa upanga wako kutoka kwa waovu. Ee Mwenyezi Mungu, mkono wako uniokoe na watu kama hawa, kutokana na watu wa ulimwengu huu ambao fungu lao liko katika maisha haya. Na wapate adhabu ya kuwatosha. Watoto wao na wapate zaidi ya hayo, hukumu na iendelee kwa watoto wa watoto wao. Bali mimi nitauona uso wako katika haki; niamkapo, nitaridhika kwa kuona sura yako.