Zaburi 17:1-15
Zaburi 17:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Ee Mwenyezi-Mungu usikie kisa changu cha haki, usikilize kilio changu, uitegee sikio sala yangu isiyo na hila. Haki yangu na ije kutoka kwako, kwani wewe wajua jambo lililo la haki. Wewe wajua kabisa moyo wangu; umenijia usiku, kunichunguza, umenitia katika jaribio; hukuona uovu ndani yangu, sikutamka kitu kisichofaa. Kuhusu matendo watendayo watu; mimi nimeitii amri yako, nimeepa njia ya wadhalimu. Nimefuata daima njia yako; wala sijateleza kamwe. Nakuita, ee Mungu, kwani wewe wanijibu; unitegee sikio, uyasikie maneno yangu. Onesha fadhili zako za ajabu, uwaokoe kutoka kwa adui zao, wale wanaokimbilia usalama kwako. Unilinde kama mboni ya jicho; unifiche kivulini mwa mabawa yako, mbali na mashambulio ya waovu, mbali na maadui zangu hatari wanaonizunguka. Hao hawana huruma yoyote moyoni; wamejaa maneno ya kujigamba. Wananifuatia na kunizunguka; wananivizia waniangushe chini. Wako tayari kunirarua kama simba: Kama mwanasimba aviziavyo mawindo. Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwakabili na kuwaporomosha. Kwa upanga uiokoe nafsi yangu kutoka kwa waovu. Kwa mkono wako, ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe mikononi mwa watu hao, watu ambao riziki yao ni dunia hii tu. Uwajaze adhabu uliyowawekea, wapate ya kuwatosha na watoto wao, wawaachie hata na wajukuu zao. Lakini mimi nitauona uso wako, kwani ni mwadilifu; niamkapo nitajaa furaha kwa kukuona.
Zaburi 17:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee BWANA, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila. Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili. Umenijaribu moyo wangu, umenijia usiku, Umenichunguza usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose, Kuhusu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu. Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kulia Uwaokoe kutoka kwa adui zao. Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya kivuli cha mbawa zako; Wasinione wasio haki wanaonionea, Adui za roho yangu wanaonizunguka. Wamejawa na ukaidi, Kwa vinywa vyao wanajigamba. Wamenifuatia; na sasa wananizunguka, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini. Kama mfano wa simba atakaye kurarua, Kama mwanasimba aoteaye katika maotea yake. Inuka, Ee BWANA, umkabili, umwangushe, Kwa upanga wako uniokoe nafsi yangu na mtu mbaya. Ee BWANA, kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu wa dunia hii ambao fungu lao liko katika maisha haya. Matumbo yao wayajaza kwa hazina yako, Hushiba wana, huwaachia watoto wao akiba zao, Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.
Zaburi 17:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee BWANA, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila. Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili. Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose, Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu. Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea. Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako; Wasinione wasio haki wanaonionea, Adui za roho yangu wanaonizunguka. Wameukaza moyo wako, Kwa vinywa vyao hutoa majivuno. Sasa wametuzunguka hatua zetu, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini. Kama mfano wa simba atakaye kurarua, Kama mwana-simba aoteaye katika maoteo yake. Ee BWANA, usimame, umkabili, umwinamishe, Kwa upanga wako uniokoe nafsi na mtu mbaya. Ee BWANA, kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu wa dunia hii ambao fungu lao li katika maisha haya. Matumbo yao wayajaza kwa hazina yako, Hushiba wana, huwaachia watoto wao akiba zao, Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.
Zaburi 17:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sikia, Ee BWANA, kusihi kwangu kwa haki, sikiliza kilio changu. Tega sikio kwa ombi langu, halitoki kwenye midomo ya udanganyifu. Hukumu yangu na itoke kwako, macho yako na yaone yale yaliyo haki. Ingawa unauchunguza moyo wangu na kunikagua usiku, ingawa umenijaribu, hutaona chochote. Nimeamua kwamba kinywa changu hakitatenda dhambi. Kuhusu matendo ya wanadamu: kwa neno la midomo yako, nimejiepusha na njia za wenye jeuri. Hatua zangu zimeshikamana na njia zako; nyayo zangu hazikuteleza. Ee Mungu, ninakuita, kwa kuwa utanijibu, nitegee sikio lako na usikie ombi langu. Uonyeshe ajabu ya upendo wako mkuu, wewe uokoaye kwa mkono wako wa kuume wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao. Nilinde kama mboni ya jicho lako, unifiche chini ya kivuli cha mbawa zako kutokana na waovu wanaonishambulia, kutokana na adui wauaji wanaonizunguka. Huifunga mioyo yao iliyo migumu, vinywa vyao hunena kwa majivuno. Wamenifuatia nyayo zangu, sasa wamenizingira, wakiwa macho, waniangushe chini. Wamefanana na simba mwenye njaa awindaye, kama simba mkubwa anyemeleaye mafichoni. Inuka, Ee BWANA, pambana nao, uwaangushe, niokoe kutokana na waovu kwa upanga wako. Ee BWANA, mkono wako uniokoe na watu wa jinsi hii, kutokana na watu wa ulimwengu huu ambao fungu lao liko katika maisha haya. Na wapate adhabu ya kuwatosha. Watoto wao na wapate zaidi ya hayo, hukumu na iendelee kwa watoto wa watoto wao. Na mimi katika haki nitauona uso wako, niamkapo, nitaridhika kwa kuona sura yako.