Zaburi 116
116
Zaburi 116
Shukrani kwa kuokolewa kutoka mauti
1Nampenda Mwenyezi Mungu kwa maana amesikia sauti yangu;
amesikia kilio changu ili anihurumie.
2Kwa sababu amenitegea sikio lake,
nitamwita siku zote za maisha yangu.
3Kamba za mauti zilinizunguka,
vitisho vya Kuzimu#116:3 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho. vilinipata,
nikalemewa na taabu na huzuni.
4Ndipo nikaliitia jina la Mwenyezi Mungu:
“Ee Mwenyezi Mungu, niokoe!”
5Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na haki,
Mungu wetu ni mwingi wa huruma.
6Mwenyezi Mungu huwalinda wanyenyekevu,
nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.
7Ee nafsi yangu, tulia tena,
kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekuwa mwema kwako.
8Kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu,
umeniokoa nafsi yangu na mauti,
macho yangu kutokana na machozi,
miguu yangu kutokana na kujikwaa,
9ili niweze kutembea mbele za Mwenyezi Mungu,
katika nchi ya walio hai.
10Nilimwamini Mwenyezi Mungu, niliposema,
“Mimi nimeteseka sana.”
11Katika taabu yangu nilisema,
“Wanadamu wote ni waongo.”
12Nimrudishie Mwenyezi Mungu nini
kwa wema wake wote alionitendea?
13Nitakiinua kikombe cha wokovu
na kulitangaza jina la Mwenyezi Mungu.
14Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Mwenyezi Mungu
mbele za watu wake wote.
15Kifo cha watakatifu kina thamani
machoni pa Mwenyezi Mungu.
16Ee Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mtumishi wako,
mimi ni mtumishi wako,
mwana wa mjakazi wako#116:16 au mwanao mwaminifu;
umeniweka huru
toka katika minyororo yangu.
17Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru
na kuliita jina la Mwenyezi Mungu.
18Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Mwenyezi Mungu
mbele za watu wake wote,
19katika nyua za nyumba ya Mwenyezi Mungu,
katikati yako, ee Yerusalemu.
Msifuni Mwenyezi Mungu.#116:19 kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 116: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.