Zaburi 105
105
Zaburi 105
Uaminifu wa Mwenyezi Mungu kwa Israeli
(1 Nyakati 16:8-22)
1Mshukuruni Mwenyezi Mungu, liitieni jina lake;
wajulisheni mataifa aliyoyatenda.
2Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa,
waambieni matendo yake yote ya ajabu.
3Lishangilieni jina lake takatifu,
mioyo ya wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu na ifurahi.
4Mtafuteni Mwenyezi Mungu na nguvu zake,
utafuteni uso wake siku zote.
5Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya,
miujiza yake na hukumu alizozitamka,
6enyi wazao wa Ibrahimu mtumishi wake,
enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
7Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Mungu wetu,
hukumu zake ziko duniani kote.
8Hulikumbuka agano lake milele,
neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
9agano alilolifanya na Ibrahimu,
kiapo alichomwapia Isaka.
10Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri,
kwa Israeli liwe agano la milele:
11“Nitakupa wewe nchi ya Kanaani
kuwa sehemu utakayoirithi.”
12Walipokuwa wachache kwa idadi,
wachache sana na wageni ndani yake,
13walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine,
kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
14Hakuruhusu mtu yeyote awadhulumu;
kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema:
15“Msiwaguse niliowapaka mafuta;
msiwadhuru manabii wangu.”
16Akaiita njaa juu ya nchi
na kuharibu chakula chao chote,
17naye akatuma mtu mbele yao,
Yusufu, aliyeuzwa kama mtumwa.
18Walichubua miguu yake kwa minyororo,
shingo yake ilifungwa kwa chuma,
19hadi yale aliyotangulia kusema yalipotimia,
hadi neno la Mwenyezi Mungu lilipomthibitisha.
20Mfalme alituma watu wakamfungua,
mtawala wa watu alimwachia huru.
21Alimfanya mkuu wa nyumba yake,
mtawala wa vyote alivyokuwa navyo,
22kuwaelekeza wakuu wa mfalme apendavyo,
na kuwafundisha wazee wake hekima.
23Kisha Israeli akaingia Misri,
Yakobo akaishi kama mgeni katika nchi ya Hamu.
24Mwenyezi Mungu aliwafanya watu wake kuzaana sana;
aliwafanya kuwa wengi sana kuliko adui zao.
25Aliigeuza mioyo yao iwachukie watu wake,
wakatenda hila dhidi ya watumishi wake.
26Akamtuma Musa mtumishi wake,
pamoja na Haruni, aliyemchagua.
27Walifanya ishara zake za ajabu miongoni mwao,
miujiza yake katika nchi ya Hamu.
28Alituma giza na nchi ikajaa giza,
kwani si walikuwa wameyaasi maneno yake?
29Aligeuza maji yao kuwa damu,
ikasababisha samaki wao kufa.
30Nchi yao ilijaa vyura tele, ambao waliingia
hadi kwenye vyumba vya kulala vya watawala wao.
31Alisema, yakaja makundi ya inzi,
na viroboto katika nchi yao yote.
32Alibadilisha mvua yao ikawa mvua ya mawe,
yenye miali ya radi nchini yao yote,
33akaharibu mizabibu yao na miti ya tini,
na akaangamiza miti ya nchi yao.
34Alisema, nzige wakaja,
tunutu wasio na idadi,
35wakala kila jani katika nchi yao,
wakala mazao ya ardhi yao.
36Kisha akawaua wazaliwa wote wa kwanza katika nchi yao,
matunda ya kwanza ya ujana wao wote.
37Akawatoa Israeli katika nchi
wakiwa na fedha na dhahabu nyingi,
wala hakuna hata mmoja
kutoka makabila yao aliyejikwaa.
38Misri ilifurahi walipoondoka,
kwa sababu hofu ya Israeli ilikuwa imewaangukia.
39Alitandaza wingu kama kifuniko,
na moto kuwamulikia usiku.
40Waliomba, naye akawaletea kware,
akawashibisha kwa mkate wa mbinguni.
41Alipasua mwamba, maji yakabubujika,
yakatiririka jangwani kama mto.
42Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu,
aliyompa Ibrahimu mtumishi wake.
43Aliwatoa watu wake kwa furaha,
wateule wake kwa kelele za shangwe,
44akawapa nchi za mataifa, wakawa warithi wa mali
ambayo wengine walikuwa wameitaabikia:
45alifanya haya ili wayashike mausia yake
na kuzitii sheria zake.
Msifuni Mwenyezi Mungu.#105:45 kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 105: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.