Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 104

104
Zaburi 104
Kumsifu Muumba
1Ee nafsi yangu, umhimidi Mwenyezi Mungu.
Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, wewe ni mkuu sana,
umejivika utukufu na enzi.
2Mwenyezi Mungu amejifunika katika nuru kama vile kwa vazi,
amezitandaza mbingu kama hema,
3na kuziweka nguzo za orofa yake juu ya maji.
Huyafanya mawingu kuwa gari lake la vita,
na hupanda kwenye mabawa ya upepo.
4Huzifanya pepo kuwa wajumbe#104:4 au malaika wake,
na miali ya moto kuwa watumishi wake.
5Ameiweka dunia kwenye misingi yake,
haiwezi kamwe kuondoshwa.
6Uliifunika kwa kilindi kama kwa vazi,
maji yalisimama juu ya milima.
7Lakini kwa kukemea kwako maji yalikimbia,
kwa sauti ya radi yako yakatoroka,
8yakapanda milima, yakateremka mabondeni,
hadi mahali pale ulipoyakusudia.
9Uliyawekea mpaka ambao hayawezi kuuvuka,
kamwe hayataifunika dunia tena.
10Huzifanya chemchemi zimwage maji mabondeni,
hutiririka kati ya milima.
11Huwapa maji wanyama wote wa kondeni,
punda-mwitu huzima kiu yao.
12Ndege wa angani hufanya viota kando ya maji,
huimba katika matawi.
13Huinyeshea milima kutoka orofa zake,
dunia inatoshelezwa kwa matunda ya kazi yake.
14Huyafanya majani ya mifugo yaote,
na mimea kwa watu kulima,
wajipatie chakula kutoka ardhini:
15divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu,
mafuta kwa ajili ya kung’arisha uso wake,
na mkate wa kutia mwili nguvu.
16Miti ya Mwenyezi Mungu inanyeshewa vizuri,
mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17Humo ndege hufanya viota vyao,
korongo ana nyumba yake kwenye msunobari.
18Milima mirefu ni makao ya mbuzi-mwitu;
majabali ni kimbilio la pelele.
19Mwezi hugawanya majira,
na jua hutambua wakati wake wa kutua.
20Unaleta giza, kunakuwa usiku,
wanyama wote wa mwituni huzurura.
21Simba hunguruma kwa mawindo yao,
na kutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.
22Jua huchomoza, nao huondoka,
hurudi na kulala katika mapango yao.
23Kisha wanadamu wanaenda kazini zao,
katika kazi zao hadi jioni.
24Ee Mwenyezi Mungu, jinsi matendo yako yalivyo mengi!
Kwa hekima ulizifanya zote,
dunia imejaa viumbe vyako.
25Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele,
imejaa viumbe visivyo na idadi,
vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo.
26Huko meli huenda na kurudi,
pia Lewiathani#104:26 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa., uliyemuumba acheze ndani yake.
27Hawa wote wanakutazamia wewe,
uwape chakula chao kwa wakati wake.
28Wakati unawapa,
wanakikusanya;
unapofumbua mkono wako,
wao wanashibishwa mema.
29Unapoficha uso wako,
wanapata hofu,
unapoondoa pumzi yao,
wanakufa na kurudi mavumbini.
30Unapopeleka Roho wako,
wanaumbwa,
nawe huufanya upya uso wa dunia.
31Utukufu wa Mwenyezi Mungu na udumu milele,
Mwenyezi Mungu na azifurahie kazi zake:
32yeye aitazamaye dunia, nayo ikatetemeka,
aigusaye milima, nayo ikatoa moshi.
33Nitamwimbia Mwenyezi Mungu maisha yangu yote;
nitaimba sifa kwa Mungu wangu muda wote ninaoishi.
34Kutafakari kwangu na kumpendeze yeye,
ninapofurahi katika Mwenyezi Mungu.
35Lakini wenye dhambi na watoweke katika dunia
na waovu wasiwepo tena.
Ee nafsi yangu, msifu Mwenyezi Mungu.
Msifuni Mwenyezi Mungu.#104:35 kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 104: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia