Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 31:20-31

Mithali 31:20-31 NENO

Huwanyooshea maskini mikono yake na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake. Theluji inaposhuka, hana hofu kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake, kwa maana wote wamevikwa nguo za kutia joto. Yeye hutengeneza mazulia ya urembo ya kufunika kitanda chake, huvaa kitani safi na urujuani. Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji, aketipo miongoni mwa wazee wa nchi. Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza, naye huwauzia wafanyabiashara mishipi. Amevikwa nguvu na heshima, anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo. Huzungumza kwa hekima, na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake. Huangalia mambo ya nyumbani mwake wala hali chakula cha uvivu. Watoto wake huamka na kumwita aliyebarikiwa, mumewe pia humsifu, akisema: “Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri, lakini wewe umewapita wote.” Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu, na uzuri unapita upesi; bali mwanamke anayemcha Mwenyezi Mungu atasifiwa. Mpe thawabu anayostahili, nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.