Mithali 14:23-35
Mithali 14:23-35 NENO
Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida, bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu. Utajiri wa wenye hekima ni taji lao, bali upumbavu wa wapumbavu huzaa upumbavu. Shahidi wa kweli huokoa maisha, bali shahidi wa uongo ni mdanganyifu. Yeye amchaye Mwenyezi Mungu ana ngome salama, na kwa watoto wake itakuwa kimbilio. Kumcha Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya uzima, ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti. Wingi wa watu ni utukufu wa mfalme, bali pasipo watu mkuu huangamia. Mtu mwenye subira ana ufahamu mwingi, bali anayekasirika haraka huonesha upumbavu. Moyo wenye amani huupa mwili uzima, bali wivu huozesha mifupa. Yeye anayemdhulumu maskini humdharau Muumba wao, bali yeyote anayemhurumia mhitaji humheshimu Mungu. Waovu huangamizwa kwa matendo yao maovu, bali hata katika kifo wenye haki hupata kimbilio. Hekima hukaa katika moyo wa mwenye ufahamu bali haijulikani miongoni mwa wapumbavu. Haki huinua taifa, bali dhambi ni aibu kwa watu wote. Mfalme hupendezwa na mtumishi mwenye hekima, bali ghadhabu yake humwangukia mtumishi mwenye kuaibisha.