Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 1

1
Utangulizi: Kusudi na kiini
1Mithali za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli:
2Kwa kupata hekima na nidhamu;
kwa kufahamu maneno ya busara;
3kwa kujipatia nidhamu na busara,
kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea;
4huwapa busara wajinga#1:4 Neno la Kiebrania lililotafsiriwa mjinga (wingi wajinga) linamaanisha mtu anayeamini chochote, asiye na maadili, na mwenye roho ya kutenda uovu.,
maarifa na akili kwa vijana;
5wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao,
wenye kupambanua na wapate mwongozo;
6kwa kufahamu mithali na mifano,
misemo na vitendawili vya wenye hekima.
7Kumcha Mwenyezi Mungu ni chanzo cha maarifa,
lakini wapumbavu#1:7 Neno la Kiebrania lililotafsiriwa mpumbavu (wingi wapumbavu) linamaanisha mtu asiye na maadili. hudharau hekima na adabu.
Maelezo juu ya hekima na upumbavu
Onyo dhidi ya ushawishi wa rafiki waovu
8Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,
wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
9Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,
na mkufu wa kuipamba shingo yako.
10Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi,
usikubaliane nao.
11Wakisema, “Twende tufuatane;
tukamvizie mtu na kumwaga damu,
njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia;
12tuwameze wakiwa hai kama kaburi#1:12 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol.,
wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni.
13Tutapata aina zote za vitu vya thamani
na kujaza nyumba zetu kwa nyara.
14Njoo ushirikiane nasi,
vitu vyote tutakavyopata tutagawana.”
15Mwanangu, usiandamane nao.
Usiweke mguu wako katika njia zao,
16kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi,
ni wepesi kumwaga damu.
17Tazama ni jinsi gani ilivyo kazi bure kutandaza wavu
wakati ndege wote wanakuona!
18Watu hawa huvizia kumwaga damu yao wenyewe;
hujivizia tu wenyewe!
19Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila;
huuondoa uhai wa wale wenye mali.
Onyo dhidi ya kukataa hekima
20Hekima huita kwa sauti kuu barabarani,
hupaza sauti yake kwenye viwanja vikubwa;
21kwenye makutano ya barabara za mji
zenye makelele mengi hupaza sauti,
kwenye malango ya mji hutoa hotuba yake:
22“Enyi wajinga, mtashikilia ujinga wenu hadi lini?
Hadi lini wenye mizaha watafurahia mizaha,
na wapumbavu kuchukia maarifa?
23Kama mngekuwa mmeitikia karipio langu,
ningekuwa nimemimina roho yangu kwenu
na kuwafahamisha maneno yangu.
24Lakini kwa kuwa mlinikataa nilipowaita
na hakuna yeyote aliyekubali
niliponyoosha mkono wangu,
25kwa kuwa mliyapuuza mashauri yangu yote
na hamkukubali karipio langu,
26mimi nami nitawacheka katika maafa yenu,
nitawadhihaki janga litakapowapata:
27janga litakapowapata kama tufani,
maafa yatakapowazoa kama upepo wa kisulisuli,
dhiki na taabu zitakapowalemea.
28“Ndipo watakaponiita lakini sitawajibu;
watanitafuta lakini hawatanipata.
29Kwa kuwa walichukia maarifa,
wala hawakuchagua kumcha Mwenyezi Mungu,
30kwa kuwa hawakukubali mashauri yangu,
na kukataa maonyo yangu,
31watakula matunda ya njia zao,
na watashibishwa matunda ya hila zao.
32Kwa kuwa ukaidi wa wajinga utawaua,
na kuridhika kwa wajinga kutawaangamiza.
33Lakini yeyote anisikilizaye ataishi kwa usalama,
atatulia, bila kuwa na hofu ya madhara.”

Iliyochaguliwa sasa

Mithali 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia