Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 25

25
Moabu yashawishi Israeli
1Israeli alipokuwa akikaa Shitimu, wanaume wa Israeli walianza kuzini na wanawake wa Moabu, 2ambao waliwaalika kushiriki katika sadaka kwa miungu yao. Watu wakala na kusujudu mbele ya miungu hiyo. 3Kwa hiyo Israeli akaungana katika kumwabudu Baali wa Peori. Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi yao.
4Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Uwachukue viongozi wote wa watu hawa, uwaue hadharani mbele za Mwenyezi Mungu, ili hasira kali ya Mwenyezi Mungu iweze kuondoka kwa Israeli.”
5Kwa hiyo Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, “Kila mmoja wenu lazima awaue wale wanaume wenu, walioshiriki katika kumwabudu Baali wa Peori.”
6Ndipo mwanaume Mwisraeli akamleta mwanamke Mmidiani katika jamaa yake palepale mbele ya Musa na mkutano wote wa Israeli walipokuwa wakilia kwenye lango la Hema la Kukutania. 7Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Haruni, alipoona jambo hili, akaondoka kwenye kusanyiko, akachukua mkuki mkononi mwake, 8akamfuata yule Mwisraeli ndani ya hema. Akawachoma mkuki wote wawili kwa pamoja, ukapenya kwenye mwili wa yule Mwisraeli na mwili wa yule mwanamke. Ndipo tauni dhidi ya Waisraeli ikakoma. 9Lakini wale waliokufa kwa hiyo tauni walikuwa watu elfu ishirini na nne.
10Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 11“Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Haruni, amegeuza hasira yangu mbali na Waisraeli, kwa sababu alikuwa na wivu kama nilio nao kwa heshima yangu miongoni mwao, hata kwamba kwa wivu wangu sikuwaangamiza. 12Kwa hiyo mwambie Finehasi ninafanya agano langu la amani naye. 13Yeye pamoja na wazao wake watakuwa na agano la ukuhani milele, kwa sababu alikuwa na wivu kwa ajili ya heshima ya Mungu wake, na akafanya upatanisho kwa Waisraeli.”
14Jina la Mwisraeli ambaye aliuawa pamoja na mwanamke Mmidiani ni Zimri mwana wa Salu, kiongozi wa jamaa ya Simeoni. 15Jina la mwanamke Mmidiani aliyeuawa ni Kozbi binti Suri, aliyekuwa mkuu wa kabila la jamaa ya Wamidiani.
16Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 17“Watendeeni Wamidiani kama adui na mwaue, 18kwa sababu wao waliwatendea kama adui wakati waliwadanganya katika tukio la Peori na dada yao Kozbi, binti ya kiongozi Mmidiani, mwanamke ambaye aliuawa wakati tauni ilikuja kama matokeo ya tukio la Peori.”

Iliyochaguliwa sasa

Hesabu 25: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia