Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 24

24
1Basi Balaamu alipoona imempendeza Mwenyezi Mungu kubariki Israeli, hakuendelea tena kutafuta uchawi kama nyakati nyingine, bali aligeuza uso wake kuelekea nyikani. 2Balaamu alipotazama nje na kuona Israeli amepiga kambi kabila kwa kabila, Roho wa Mungu akawa juu yake, 3naye akatoa ujumbe wake:
“Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori,
ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri;
4ujumbe wake yeye anayesikia maneno ya Mungu,
anayeona maono kutoka kwa Mwenyezi#24:4 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania (pia 24:16).,
ambaye husujudu, na macho yake yamefunguka:
5“Tazama jinsi yalivyo mazuri mahema yako, ee Yakobo,
maskani zako, ee Israeli!
6“Kama mabonde, yanaenea,
kama bustani kando ya mto,
kama miti ya udi iliyopandwa na Mwenyezi Mungu,
kama mierezi kando ya maji.
7Maji yatatiririka kutoka ndoo zake;
mbegu yake itakuwa na maji tele.
“Mfalme wake atakuwa mkuu kuliko Mfalme Agagi;
ufalme wake utatukuka.
8“Mungu alimleta kutoka Misri;
yeye ana nguvu kama nyati.
Anayararua mataifa yaliyo adui zake,
na kuvunja mifupa yao vipande vipande;
huwachoma kwa mishale yake.
9Hujikunyata na kuvizia kama simba,
kama simba jike; nani anayethubutu kumwamsha?
“Abarikiwe kila akubarikiye,
na alaaniwe kila akulaaniye!”
10Ndipo hasira ya Balaki ikawaka dhidi ya Balaamu. Akapiga mikono yake pamoja, akamwambia Balaamu, “Nilikuita uje kuwalaani adui zangu, lakini umewabariki mara hizi tatu. 11Sasa ondoka upesi uende nyumbani! Mimi nilisema nitakuzawadia vizuri sana, lakini Mwenyezi Mungu amekuzuia usizawadiwe.”
12Balaamu akamwambia Balaki, “Je, hukumbuki jinsi nilivyowaambia wajumbe uliowatuma kwangu? Niliwaambia hivi, 13‘Hata ikiwa Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, nisingeweza kufanya kitu chochote kwa matakwa yangu, kikiwa kizuri au kibaya, kwenda kinyume na agizo la Mwenyezi Mungu, nami imenipasa kusema tu kile Mwenyezi Mungu atakachosema’? 14Sasa ninarudi kwa watu wangu. Lakini njoo, nikuonye kuhusu kile watu hawa watakachowatenda watu wako siku zijazo.”
Ujumbe wa nne wa Balaamu
15Kisha Balaamu akatoa ujumbe wake:
“Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori,
ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri;
16ujumbe wake yeye ambaye husikia maneno ya Mungu,
mwenye maarifa kutoka kwa Aliye Juu Sana,
aonaye maono kutoka kwa Mwenyezi,
na kuanguka kifudifudi
nayo macho yake yamefunguliwa:
17“Namwona yeye, lakini si sasa;
namtazama yeye, lakini si karibu.
Nyota itatoka kwa Yakobo,
fimbo ya ufalme itainuka kutoka kwa Israeli.
Atawaponda Wamoabu paji za nyuso,
na mafuvu yote ya wana wa Shethi.
18Edomu itamilikiwa,
Seiri, adui yake, itamilikiwa,
lakini Israeli atakuwa na nguvu.
19Mtawala atakuja kutoka kwa Yakobo
na kuangamiza walionusurika katika mji.”
Ujumbe wa mwisho wa Balaamu
20Kisha Balaamu akawaona watu wa Amaleki, na kutoa ujumbe wake:
“Amaleki alikuwa ya kwanza miongoni mwa mataifa,
lakini mwisho wake ataangamizwa milele.”
21Kisha akawaona Wakeni, akatoa ujumbe wake:
“Makao yenu ni salama,
kiota chenu kiko kwenye mwamba.
22Hata hivyo ninyi Wakeni mtaangamizwa
Ashuru atakapowachukua mateka.”
23Ndipo akatoa ujumbe wake:
“Ole wao! Ni nani ataweza kuishi Mungu atakapofanya hili?
24Meli zitakuja kutoka pwani za Kitimu,
zitaitiisha Ashuru na Eberi,
lakini nao pia wataangamizwa.”
25Kisha Balaamu akainuka na kurudi nyumbani mwake, naye Balaki akashika njia yake.

Iliyochaguliwa sasa

Hesabu 24: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia