Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 23

23
Ujumbe wa kwanza wa Balaamu
1Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, mnitayarishie mafahali saba na kondoo dume saba.” 2Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema; hao wawili kila mmoja wao akatoa fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.
3Kisha Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati mimi ninaenda kando. Huenda Mwenyezi Mungu atakuja kukutana nami. Lolote atakalonifunulia, nitakuambia.” Basi akaenda hata mahali peupe palipoinuka.
4Mungu akakutana naye, kisha Balaamu akasema, “Nimekwisha kutengeneza madhabahu saba, na juu ya kila madhabahu nimetoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja.”
5Mwenyezi Mungu akaweka ujumbe katika kinywa cha Balaamu na kusema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”
6Basi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake akiwa na wakuu wote wa Moabu. 7Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake:
“Balaki amenileta kutoka Aramu,
mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki.
Akasema, ‘Njoo, unilaanie Yakobo;
njoo unishutumie Israeli.’
8Nitawezaje kuwalaani,
hao ambao Mungu hajawalaani?
Nitawezaje kuwashutumu
hao ambao Mwenyezi Mungu hakuwashutumu?
9Kutoka vilele vya miamba ninawaona,
kutoka mahali palipoinuka ninawatazama.
Ninaliona taifa ambalo wanaishi peke yao,
nao hawahesabiwi kama mojawapo ya mataifa.
10Ni nani awezaye kuhesabu mavumbi ya Yakobo,
au kuhesabu robo ya Israeli?
Mimi na nife kifo cha mtu mwenye haki,
na mwisho wangu na uwe kama wao!”
11Balaki akamwambia Balaamu, “Ni nini ulichonitendea? Nimekuleta ulaani adui zangu, lakini wewe badala yake umewabariki!”
12Balaamu akajibu, “Je, hainipasi kusema kile Mwenyezi Mungu anachoweka katika kinywa changu?”
Ujumbe wa pili wa Balaamu
13Ndipo Balaki akamwambia, “Twende pamoja mahali pengine ambapo unaweza kuwaona; utawaona baadhi tu wala si wote. Nawe kutoka huko, unilaanie hao.” 14Basi akampeleka kwenye shamba la Sofimu, juu ya kilele cha Mlima Pisga. Pale akajenga madhabahu saba na kutoa sadaka ya fahali na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.
15Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati ninapoenda kuonana na Mungu kule.”
16Mwenyezi Mungu akakutana na Balaamu, akaweka ujumbe katika kinywa chake akasema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”
17Basi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake, akiwa na wakuu wa Moabu. Balaki akamuuliza, “Je, Mwenyezi Mungu amesema nini?”
18Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake:
“Balaki, inuka na usikilize,
nisikie mimi, wewe mwana wa Sipori.
19Mungu si mtu, hata aseme uongo,
wala yeye si mwanadamu, hata ajute.
Je, anasema, kisha asitende?
Je, anaahidi, asitimize?
20Nimepokea agizo kubariki;
amebariki, nami siwezi kubadilisha.
21“Haijaonekana bahati mbaya katika Yakobo,
wala taabu katika Israeli.
Mwenyezi Mungu, Mungu wao, yu pamoja nao,
nayo sauti kuu ya Mfalme imo kati yao.
22Mungu aliwatoa kutoka Misri;
wao wana nguvu kama za nyati.
23Hakuna uchawi dhidi ya Yakobo,
wala hakuna uaguzi dhidi ya Israeli.
Sasa itasemwa kuhusu Yakobo
na Israeli, ‘Tazama yale Mungu aliyotenda!’
24Taifa lainuka kama simba jike;
linajiinua kama simba
ambaye hatulii hadi amalize kurarua mawindo yake
na kunywa damu ya mawindo yake.”
25Kisha Balaki akamwambia Balaamu, “Usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa!”
26Balaamu akajibu, “Je, sikukuambia ni lazima nifanye lolote analosema Mwenyezi Mungu?”
Ujumbe wa tatu wa Balaamu
27Basi Balaki akamwambia Balaamu, “Njoo, nikupeleke mahali pengine. Huenda itampendeza Mungu kukuruhusu unilaanie hao watu kutoka mahali hapo.” 28Balaki akamchukua Balaamu juu ya Mlima Peori, unaotazamana na nyika.
29Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, uandae mafahali saba na kondoo dume saba kwa ajili yangu.” 30Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, kisha akatoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.

Iliyochaguliwa sasa

Hesabu 23: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia