Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 1

1
Watu wahesabiwa kwa mara ya kwanza
1Mwenyezi Mungu alisema na Musa katika Jangwa la Sinai, katika Hema la Kukutania, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, katika mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri. Akamwambia, 2“Hesabu watu wa jumuiya yote ya Waisraeli kwa kufuata koo zao na jamaa zao, ukiorodhesha kila mwanaume kwa jina lake, mmoja mmoja. 3Wewe na Haruni mtawahesabu kwa migawanyo yao wanaume wote katika Israeli wenye miaka ishirini na kuendelea wanaoweza kutumika katika jeshi. 4Mwanaume mmoja kutoka kila kabila, kila aliye kiongozi wa jamaa yake, atawasaidia.
5“Haya ndiyo majina ya wanaume watakaowasaidia:
“kutoka Reubeni, ni Elisuri mwana wa Shedeuri;
6kutoka Simeoni, ni Shelumieli mwana wa Surishadai;
7kutoka Yuda, ni Nashoni mwana wa Aminadabu;
8kutoka Isakari, ni Nethaneli mwana wa Suari;
9kutoka Zabuloni, ni Eliabu mwana wa Heloni;
10kutoka wana wa Yusufu:
kutoka Efraimu, ni Elishama mwana wa Amihudi;
kutoka Manase, ni Gamalieli mwana wa Pedasuri;
11kutoka Benyamini, ni Abidani mwana wa Gideoni;
12kutoka Dani, ni Ahiezeri mwana wa Amishadai;
13kutoka Asheri, ni Pagieli mwana wa Okrani;
14kutoka Gadi, ni Eliasafu mwana wa Deueli;
15kutoka Naftali, ni Ahira mwana wa Enani.”
16Hawa walikuwa wanaume walioteuliwa kutoka jumuiya, viongozi wa makabila ya baba zao. Walikuwa wakuu wa koo za Israeli.
17Musa na Haruni wakawachukua wanaume hao waliokuwa wamepewa majina yao, 18wakaita jumuiya yote pamoja katika siku ya kwanza ya mwezi wa pili. Watu wakaonesha nasaba zao kwa koo zao na jamaa zao, nao wanaume waliokuwa na miaka ishirini au zaidi waliorodheshwa kwa majina, mmoja mmoja, 19kama Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa. Hivyo aliwahesabu katika Jangwa la Sinai:
20Kutoka wazao wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Israeli:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, mmoja mmoja, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 21Idadi kutoka kabila la Reubeni ilikuwa watu elfu arobaini na sita na mia tano.
22Kutoka wazao wa Simeoni:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi walihesabiwa na kuorodheshwa kwa majina, mmoja mmoja, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 23Idadi kutoka kabila la Simeoni walikuwa watu elfu hamsini na tisa na mia tatu.
24Kutoka wazao wa Gadi:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 25Idadi kutoka kabila la Gadi walikuwa watu elfu arobaini na tano, mia sita na hamsini.
26Kutoka wazao wa Yuda:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 27Idadi kutoka kabila la Yuda walikuwa watu elfu sabini na nne na mia sita.
28Kutoka wazao wa Isakari:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 29Idadi kutoka kabila la Isakari walikuwa watu elfu hamsini na nne na mia nne.
30Kutoka wazao wa Zabuloni:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 31Idadi kutoka kabila la Zabuloni walikuwa watu elfu hamsini na saba na mia nne.
32Kutoka wana wa Yusufu:
Kutoka wazao wa Efraimu:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 33Idadi kutoka kabila la Efraimu walikuwa watu elfu arobaini na mia tano.
34Kutoka wazao wa Manase:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 35Idadi kutoka kabila la Manase walikuwa watu elfu thelathini na mbili na mia mbili.
36Kutoka wazao wa Benyamini:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 37Idadi kutoka kabila la Benyamini walikuwa watu elfu thelathini na tano na mia nne.
38Kutoka wazao wa Dani:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 39Idadi kutoka kabila la Dani walikuwa watu elfu sitini na mbili na mia saba.
40Kutoka wazao wa Asheri:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 41Idadi kutoka kabila la Asheri walikuwa watu elfu arobaini na moja na mia tano.
42Kutoka wazao wa Naftali:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 43Idadi kutoka kabila la Naftali walikuwa watu elfu hamsini na tatu na mia nne.
44Hawa walikuwa wanaume waliohesabiwa na Musa, Haruni na viongozi kumi na wawili wa Israeli, kila mmoja akiwakilisha jamaa yake. 45Wanaume wote Waisraeli waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi la Israeli walihesabiwa kufuatana na jamaa zao. 46Jumla ya hesabu yao ilikuwa watu elfu mia sita na tatu mia tano na hamsini (603,550).
47Hata hivyo, jamaa ya kabila la Lawi hawakuhesabiwa pamoja na wengine. 48Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Musa: 49“Kamwe usihesabu kabila la Lawi wala kuwaweka pamoja katika hesabu ya Waisraeli wengine. 50Badala yake, waweke Walawi kuwa viongozi wa Maskani ya Ushuhuda, juu ya samani zake na kila kitu kilicho ndani yake. Wao watabeba Maskani na samani zake zote; wataitunza na kupiga kambi kuizunguka. 51Wakati wowote Maskani inapohamishwa, Walawi wataifungua, na wakati wowote Maskani inapotakiwa kusimamishwa, Walawi watafanya kazi hiyo. Mtu yeyote mwingine ambaye atasogea karibu nayo atauawa. 52Waisraeli watapiga mahema yao kwa makundi makundi, kila mwanaume katika kambi yake mwenyewe chini ya bendera yake. 53Hata hivyo, Walawi watapiga mahema yao kuzunguka Maskani ya Ushuhuda ili ghadhabu isiipate jumuiya ya Waisraeli. Walawi watawajibika kwa utunzaji wa Maskani ya Ushuhuda.”
54Waisraeli walifanya haya yote kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.

Iliyochaguliwa sasa

Hesabu 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia