Marko 9
9
1Isa akaendelea kuwaambia, “Amin, nawaambia, kuna watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu.”
Isa abadilika sura
(Mathayo 17:1-13; Luka 9:28-36)
2Baada ya siku sita, Isa akawachukua Petro, Yakobo na Yohana, akawapeleka juu ya mlima mrefu, mahali walipokuwa faraghani. Huko, Isa akageuka sura mbele yao. 3Mavazi yake yakawa na weupe wa kuzima macho, meupe kuliko vile mtu yeyote duniani angeweza kuyang’arisha. 4Musa na Ilya wakawatokea, wakawa wanazungumza na Isa.
5Petro akamwambia Isa, “Mwalimu, ni vyema sisi tukae hapa. Turuhusu tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Ilya.” 6Petro hakujua aseme nini kwa maana yeye na wenzake walikuwa wameogopa sana.
7Ndipo pakatokea wingu, likawafunika, nayo sauti kutoka lile wingu ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Msikieni yeye.”
8Mara walipotazama huku na huku, hawakuona tena mtu mwingine yeyote pamoja nao isipokuwa Isa.
9Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Isa akawakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, hadi Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu. 10Wakalihifadhi jambo hilo wao wenyewe, lakini wakawa wanajiuliza, “Huku kufufuka kwa wafu maana yake nini?”
11Wakamuuliza, “Kwa nini walimu wa Torati husema kwamba ni lazima Ilya aje kwanza?”
12Isa akawajibu, “Ni kweli, Ilya yuaja kwanza ili kutengeneza mambo yote. Mbona basi imeandikwa kwamba Mwana wa Adamu ni lazima ateseke sana na kudharauliwa? 13Lakini nawaambia, Ilya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyopenda, kama ilivyoandikwa kumhusu.”
Isa amponya kijana mwenye pepo mchafu
(Mathayo 17:14-21; Luka 9:37-45)
14Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa Torati wakibishana nao. 15Mara wale watu walipomwona Isa, wakastaajabu sana, wakamkimbilia ili kumsalimu.
16Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?”
17Mtu mmoja miongoni mwa umati ule wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anayemfanya asiweze kuongea. 18Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”
19Isa akawaambia, “Enyi kizazi kisichoamini! Nitakuwa pamoja nanyi hadi lini? Nitawavumilia hadi lini? Mleteni mvulana kwangu.”
20Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Isa, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.
21Isa akamuuliza baba yake, “Mwanao amekuwa katika hali hii tangu lini?”
Akamjibu, “Tangu utoto wake. 22Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lolote, tafadhali tuhurumie utusaidie.”
23Isa akamwambia, “Ati, ‘Kama unaweza kufanya jambo lolote’? Yote yawezekana kwake yeye aaminiye.”
24Mara baba yake yule mvulana akapaza sauti akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!”
25Isa alipoona kwamba umati wa watu wanakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke, wala usimwingie tena!”
26Baada ya yule pepo mchafu kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.” 27Lakini Isa akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.
28Baada ya Isa kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo mchafu?”
29Isa akawajibu, “Pepo aina hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba [na kufunga]#9:29 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya..”
Isa atabiri tena kifo chake na ufufuo
(Mathayo 17:22-23; Luka 9:43-45)
30Wakaondoka huko, wakapitia Galilaya. Isa hakutaka mtu yeyote afahamu mahali walipo, 31kwa maana alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu. Nao watamuua, lakini siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.” 32Lakini wao hawakuelewa kile alimaanisha, nao waliogopa kumuuliza maana yake.
Aliye mkuu katika Ufalme wa mbinguni
(Mathayo 18:1-5; Luka 9:46-48; 22:24-30)
33Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini kule njiani?” 34Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu zaidi ya wote.
35Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili, akawaambia: “Kama mtu yeyote akitaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”
36Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha katikati yao. Akamkumbatia, akawaambia, 37“Mtu yeyote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha Baba#9:37 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu aliyenituma.”
Yeyote asiye kinyume nasi yuko upande wetu
(Luka 9:49-50)
38Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamkataza, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”
39Isa akasema, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna yeyote atendaye miujiza kwa Jina langu ambaye baada ya kitambo kidogo aweza kunena lolote baya dhidi yangu. 40Kwa maana yeyote asiye kinyume chetu, yuko upande wetu. 41Amin, nawaambia, yeyote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Al-Masihi, hakika hataikosa thawabu yake.
Kujaribiwa ili kutenda dhambi
(Mathayo 18:6-9; Luka 17:1-2)
42“Mtu yeyote akimsababisha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa baharini. 43Mkono wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili lakini ukaingia Jehanamu, mahali ambako moto hauzimiki. [ 44Ni mahali ambako funza wao hawafi wala moto wao hauzimiki.]#9:44 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya. 45Mguu wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili lakini ukaingia Jehanamu. [ 46Ni mahali ambako funza wao hawafi wala moto wao hauzimiki.]#9:46 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya. 47Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, ling’oe. Ni afadhali kwako kuingia katika ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa Jehanamu. 48Ni mahali ambako funza wao hawafi, wala moto wao hauzimiki.#9:48 Isaya 66:24
49Kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.
50“Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utaifanyaje ili iweze kukolea tena? Mwe na chumvi ndani yenu, mkaishi kwa amani, kila mmoja na mwenzake.”
Iliyochaguliwa sasa
Marko 9: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.