Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 10

10
Safari ya kwenda Yerusalemu na matukio mjini
(Marko 10:1–12:44)
Isa afundisha kuhusu talaka
(Mathayo 19:1-12; Luka 16:18)
1Isa akaondoka huko, akavuka Mto Yordani, akaenda sehemu za Yudea. Umati mkubwa wa watu wakaenda kwake tena, naye akawafundisha, kama ilivyokuwa desturi yake.
2Baadhi ya Mafarisayo#10:2 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. wakaja ili kumjaribu kwa kumuuliza, “Je, ni halali mtu kumwacha mke wake?”
3Isa akawajibu, “Je, Musa aliwaamuru nini?”
4Wakajibu, “Musa aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”
5Isa akawaambia, “Musa aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. 6Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke’#10:6 Mwanzo 1:27. 7‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, 8na hao wawili watakuwa mwili mmoja.’#10:8 Mwanzo 2:24 Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena, bali mwili mmoja. 9Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”
10Walipokuwa tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza kuhusu jambo hili. 11Akawajibu, “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine, anazini naye. 12Naye mwanamke amwachaye mumewe na kuolewa na mume mwingine, anazini.”
Isa awabariki watoto wadogo
(Mathayo 19:13-15; Luka 18:15-17)
13Watu walikuwa wakimletea Isa watoto wadogo ili awaguse, lakini wanafunzi wake wakawakemea. 14Isa alipoona yaliyokuwa yakitukia, akachukizwa. Akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa. 15Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.” 16Akawachukua watoto mikononi mwake, akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.
Kijana tajiri
(Mathayo 19:16-30; Luka 18:18-30)
17Isa alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
18Isa akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake. 19Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’#10:19 Kutoka 20:12-16; Kumbukumbu 5:16-20
20Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
21Isa akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
22Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana. Akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23Isa akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Itakuwa vigumu sana kwa wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!”
24Wanafunzi wake wakashangazwa sana na maneno hayo. Lakini Isa akawaambia tena, “Wanangu, tazama jinsi ilivyo vigumu kwa wale wanaotumainia mali kuingia katika ufalme wa Mungu. 25Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
26Wanafunzi wake wakashangaa sana. Wakaulizana wao kwa wao, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
27Isa akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu sivyo. Mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”
28Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha kila kitu na kukufuata wewe!”
29Isa akasema, “Amin, nawaambia, hakuna mtu yeyote aliyeacha nyumba, ndugu wa kiume au wa kike, au mama au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, 30ambaye hatalipwa mara mia katika ulimwengu huu: nyumba, ndugu wa kiume na wa kike, mama na baba na watoto, mashamba pamoja na mateso, kisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao. 31Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na wa mwisho watakuwa wa kwanza.”
Isa atabiri tena kifo chake
(Mathayo 20:17-19; Luka 18:31-34)
32Walikuwa njiani wakipanda kwenda Yerusalemu, na Isa alikuwa amewatangulia. Wanafunzi wake walishangaa, nao watu waliowafuata walijawa na hofu. Isa akawachukua tena wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia yatakayompata. 33Akasema, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atasalitiwa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa Torati. Wao watamhukumu kifo na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa, 34ambao watamdhihaki na kumtemea mate, watampiga na kumuua. Siku tatu baadaye atafufuka.”
Ombi la Yakobo na Yohana
(Mathayo 20:20-28)
35Kisha Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakaja kwake na kumwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie lolote tutakalokuomba.”
36Naye akawaambia, “Je, mwataka niwafanyie jambo gani?”
37Wakamwambia, “Tupe kukaa mmoja upande wako wa kuume na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.”
38Lakini Isa akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?”
39Wakajibu, “Tunaweza.”
Kisha Isa akawaambia, “Kikombe nikinyweacho mtakinywea na ubatizo nibatizwao mtabatizwa, 40lakini kuketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto si juu yangu mimi kuwapa. Nafasi hizi ni kwa ajili ya wale walioandaliwa.”
41Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana. 42Lakini Isa akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa wale wanaodhaniwa kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu, nao wenye vyeo huonesha mamlaka yao. 43Lakini isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 44na yeyote anayetaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa mtumwa wa wote. 45Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
Isa amponya kipofu Bartimayo
(Mathayo 20:29-34; Luka 18:35-43)
46Kisha wakafika Yeriko. Isa alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mmoja, jina lake Bartimayo (maana yake “mwana wa Timayo”), alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada. 47Aliposikia kuwa ni Isa Al-Nasiri aliyekuwa anapita, akaanza kupaza sauti akisema, “Isa, Mwana wa Daudi#10:47 Ina maana kwamba Isa ni mrithi wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu (Zaburi 89:3-4)., nihurumie!”
48Watu wengi wakamkemea, wakamwambia akae kimya, lakini yeye akazidi kupaza sauti, akisema, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”
49Isa akasimama na kusema, “Mwiteni.”
Hivyo wakamwita yule mtu kipofu, wakamwambia, “Jipe moyo! Inuka, anakuita.” 50Akiwa analivua lile joho lake, alisimama na kumwendea Isa.
51Isa akamuuliza, “Unataka nikufanyie nini?”
Yule kipofu akajibu, “Mwalimu, nataka kuona.”
52Isa akamwambia, “Nenda zako, imani yako imekuponya.” Mara akapata kuona, akamfuata Isa njiani.

Iliyochaguliwa sasa

Marko 10: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia