Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 9:38-50

Marko 9:38-50 NENO

Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamkataza, kwa sababu yeye si mmoja wetu.” Isa akasema, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna yeyote atendaye miujiza kwa Jina langu ambaye baada ya kitambo kidogo aweza kunena lolote baya dhidi yangu. Kwa maana yeyote asiye kinyume chetu, yuko upande wetu. Amin, nawaambia, yeyote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Al-Masihi, hakika hataikosa thawabu yake. “Mtu yeyote akimsababisha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa baharini. Mkono wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili lakini ukaingia Jehanamu, mahali ambako moto hauzimiki. [ Ni mahali ambako funza wao hawafi wala moto wao hauzimiki.] Mguu wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili lakini ukaingia Jehanamu. [ Ni mahali ambako funza wao hawafi wala moto wao hauzimiki.] Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, ling’oe. Ni afadhali kwako kuingia katika ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa Jehanamu. Ni mahali ambako funza wao hawafi, wala moto wao hauzimiki. Kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto. “Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utaifanyaje ili iweze kukolea tena? Mwe na chumvi ndani yenu, mkaishi kwa amani, kila mmoja na mwenzake.”