Mk 9:38-50
Mk 9:38-50 SUV
Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu. Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake. Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini. Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; [ ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.] Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; [ ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.] Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto. Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi.