Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 8:1-7, 9-21

Marko 8:1-7 NEN

Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Ninauhurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula. Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.” Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?” Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?” Wakajibu, “Tuna mikate saba.” Akawaambia watu waketi chini. Akiisha kuichukua mikate saba na kushukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo. Walikuwa pia na visamaki vichache, Yesu akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu.

Marko 8:9-21 NEN

Watu waliokula walikuwa wapata 4,000. Akiisha kuwaaga, aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha. Mafarisayo wakaja, wakaanza kumhoji Yesu. Ili kumtega, wakamwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni. Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin nawaambieni, hakitapewa ishara yoyote.” Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ngʼambo. Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate ya kutosha. Walikuwa na mkate mmoja tu kwenye mashua. Yesu akawaonya: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.” Wakajadiliana wao kwa wao, na kusema, “Anasema hivi kwa sababu hatukuleta mikate.” Yesu, akifahamu majadiliano yao, akawauliza: “Mbona mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Je, bado hamtambui wala hamwelewi? Je, mbona mioyo yenu ni migumu kiasi hicho? Je, mna macho lakini mnashindwa kuona, na mna masikio lakini mnashindwa kusikia? Je, hamkumbuki? Nilipoimega ile mikate mitano kuwalisha watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa vya masazo?” Wakamjibu, “Kumi na viwili.” “Je, nilipoimega ile mikate saba kuwalisha watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa vya masazo?” Wakamjibu, “Saba.” Ndipo akawauliza, “Je, bado hamwelewi?”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Marko 8:1-7, 9-21

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha