Marko 8:1-7,9-21
Marko 8:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena, na hawakuwa na chakula. Basi, Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa watazimia njiani, maana baadhi yao wametoka mbali.” Wanafunzi wake wakamwuliza, “Hapa nyikani itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba.” Basi, akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia. Walikuwa pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki, akaamuru vigawiwe watu vilevile.
Marko 8:9-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Nao waliokula walikuwa watu wapatao 4,000. Yesu akawaaga, na mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha. Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka afanye ishara kutoka mbinguni. Yesu akahuzunika rohoni, akasema, “Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote.” Basi, akawaacha, akapanda tena mashua, akaanza safari kwenda ngambo ya pili ya ziwa. Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika mashua. Yesu akawaonya, “Angalieni sana! Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.” Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao, “Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate.” Yesu alitambua hayo, akawaambia, “Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu ni mizito? Je, mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu 5,000? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki.” Wakamjibu, “Kumi na viwili.” “Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki?” Wakamjibu, “Saba.” Basi, akawaambia, “Na bado hamjaelewa?”
Marko 8:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula; nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao wakiwa na njaa, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali. Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani? Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandalie; wakawaandalia mkutano. Walikuwa na visamaki vichache; akavibariki, akasema wawagawie na hivyo pia.
Marko 8:9-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na watu waliokula walikuwa elfu nne. Akawaaga. Mara akapanda katika mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha. Wakatokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana naye; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu. Akapiga kite rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki. Akawaacha, akapanda tena katika mashua, akaenda zake hadi ng'ambo. Wakasahau kuchukua mikate, wala katika mashua hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate. Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili. Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Saba. Akawaambia, Hamjafahamu bado?
Marko 8:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia, “Ninauhurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula. Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.” Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?” Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?” Wakajibu, “Tuna mikate saba.” Akawaambia watu waketi chini. Akiisha kuichukua mikate saba na kushukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo. Walikuwa pia na visamaki vichache, Yesu akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu.
Marko 8:9-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Watu waliokula walikuwa wapata 4,000. Akiisha kuwaaga, aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha. Mafarisayo wakaja, wakaanza kumhoji Yesu. Ili kumtega, wakamwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni. Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin nawaambieni, hakitapewa ishara yoyote.” Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ngʼambo. Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate ya kutosha. Walikuwa na mkate mmoja tu kwenye mashua. Yesu akawaonya: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.” Wakajadiliana wao kwa wao, na kusema, “Anasema hivi kwa sababu hatukuleta mikate.” Yesu, akifahamu majadiliano yao, akawauliza: “Mbona mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Je, bado hamtambui wala hamwelewi? Je, mbona mioyo yenu ni migumu kiasi hicho? Je, mna macho lakini mnashindwa kuona, na mna masikio lakini mnashindwa kusikia? Je, hamkumbuki? Nilipoimega ile mikate mitano kuwalisha watu 5,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa vya masazo?” Wakamjibu, “Kumi na viwili.” “Je, nilipoimega ile mikate saba kuwalisha watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa vya masazo?” Wakamjibu, “Saba.” Ndipo akawauliza, “Je, bado hamwelewi?”
Marko 8:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula; nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali. Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani? Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; wakawaandikia mkutano. Walikuwa na visamaki vichache; akavibarikia, akasema wawaandikie na hivyo pia.
Mk 8:9-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga. Mara akapanda chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha. Wakatokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana naye; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu. Akaugua rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki. Akawaacha, akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng’ambo. Wakasahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate. Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili. Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, Saba. Akawaambia, Hamjafahamu bado?