Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 14:12-13, 15-31

Marko 14:12-13 NEN

Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo kwa desturi mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wa Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?” Basi akawatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni mjini. Huko mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni.

Marko 14:15-31 NEN

Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kilichopambwa tena kilicho tayari. Tuandalieni humo.” Wale wanafunzi wakaondoka na kwenda mjini, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka. Ilipofika jioni, Yesu akaja pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. Walipoketi mezani wakila, Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti, mmoja anayekula pamoja nami.” Wakaanza kuhuzunika na kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?” Akawajibu, “Ni mmoja miongoni mwenu ninyi kumi na wawili, yule anayechovya mkate kwenye bakuli pamoja nami. Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa.” Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni mle; huu ndio mwili wangu.” Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, nao wote wakanywa kutoka humo. Akawaambia, “Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia, sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya katika Ufalme wa Mungu.” Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni. Yesu akawaambia, “Ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa: “ ‘Nitampiga mchungaji, nao kondoo watatawanyika.’ Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.” Petro akasema, “Hata kama wengine wote watakuacha, mimi sitakuacha.” Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia; leo, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, wewe mwenyewe utanikana mara tatu.” Lakini Petro akasisitiza zaidi, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Marko 14:12-13, 15-31

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha