Marko 10:1-12
Marko 10:1-12 NENO
Isa akaondoka huko, akavuka Mto Yordani, akaenda sehemu za Yudea. Umati mkubwa wa watu wakaenda kwake tena, naye akawafundisha, kama ilivyokuwa desturi yake. Baadhi ya Mafarisayo wakaja ili kumjaribu kwa kumuuliza, “Je, ni halali mtu kumwacha mke wake?” Isa akawajibu, “Je, Musa aliwaamuru nini?” Wakajibu, “Musa aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.” Isa akawaambia, “Musa aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke’. ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.’ Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena, bali mwili mmoja. Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” Walipokuwa tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza kuhusu jambo hili. Akawajibu, “Mtu yeyote amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine, anazini naye. Naye mwanamke amwachaye mumewe na kuolewa na mume mwingine, anazini.”