Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 5:1-16

Mathayo 5:1-16 NEN

Basi Yesu alipoona makutano, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia. Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema: “Heri walio maskini wa roho, maana Ufalme wa Mbinguni ni wao. Heri wale wanaohuzunika, maana hao watafarijiwa. Heri walio wapole, maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watatoshelezwa. Heri wenye huruma, maana hao watapata rehema. Heri walio na moyo safi, maana hao watamwona Mungu. Heri walio wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki, maana Ufalme wa Mbinguni ni wao. “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu. “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu. “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mathayo 5:1-16