Mathayo 23:23-39
Mathayo 23:23-39 NENO
“Ole wenu walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani haki, huruma na uaminifu. Iliwapasa kufanya haya makuu ya sheria bila kupuuza hayo matoleo. Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia! “Ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu! Safisha ndani ya kikombe na sahani kwanza, ndipo nje itakuwa safi pia. “Ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje, lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu. “Ole wenu, walimu wa Torati na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki. Nanyi mwasema, ‘Kama tungeishi wakati wa baba zetu, hatungeshiriki katika kumwaga damu ya manabii!’ Hivyo mnajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii. Haya basi, kijazeni kipimo cha dhambi ya baba zenu! “Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya Jehanamu? Kwa sababu hii, tazameni, natuma kwenu manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwasulubisha, na wengine wao mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na kuwafuatia kutoka mji mmoja hadi mji mwingine. Hivyo ile damu ya wenye haki wote iliyomwagwa hapa duniani, tangu damu ya Habili, aliyekuwa mwenye haki, hadi damu ya Zakaria mwana wa Barakia, mliyemuua kati ya patakatifu na madhabahu, itawajia juu yenu. Amin, nawaambia, haya yote yatakuja kwa kizazi hiki. “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka! Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. Kwa maana nawaambia, hamtaniona tena tangu sasa hadi mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu.’”